Loading...

Mtalii afariki dunia akipanda Mlima Kilimanjaro.

RAIA wa Norway Johan Aclep (54), amefariki dunia katika eneo la Kempu ya Simba iliyopo Rongai Wilaya ya Rombo, baada ya kuugua ghafla wakati akipanda Mlima Kilimanjaro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa, alisema mtalii huyo alipoteza maisha Desemba 31, mwaka huu, majira ya saa 9:30 alasiri, baada ya kupanda kupitia lango la Rongai, lililopo Wilaya ya Rombo.

“Huyo mgeni aliugua ghafla na kufariki dunia akiwa maeneo ya Simba Camp, wakati anapanda Mlima Kilimanjaro, Jumamosi ya Desemba 31, mwaka jana,” alisema.

Mtalii huyo aliingia nchini Desemba 29, mwaka 2016, akiwa anatumia hati ya kusafiria namba 28890496 kwa ajili ya kupanda mlima huo.

Kwa mujibu Mutafungwa, mwili wa mtalii huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya KCMC, ukisubiri uchunguzi wa kitabibu pamoja na taratibu nyingine za kiserikali.

Mwaka 2013, Mlima Kilimanjaro uliingia katika orodha ya maajabu saba ya asili ya Afrika. Kilele cha Kibo chenye urefu wa mita 5,895, ndicho kivutio kikubwa kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi kutokana na kufunikwa na theluji.

Safari ya kuupanda huo mlima, humpitisha mpandaji katika kanda za hali ya hewa tofauti kuanzia ile ya nchi za kitropiki hadi arkitiki.

Katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, kuna njia sita za kupanda hadi kileleni na njia iliyo rahisi na iliyo maarufu zaidi ni ile ya kuanzia lango la Marangu ambako ndiyo makao makuu ya hifadhi.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Mtalii afariki dunia akipanda Mlima Kilimanjaro.  Mtalii afariki dunia akipanda Mlima Kilimanjaro. Reviewed by Zero Degree on 1/03/2017 08:55:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.