Loading...

Mvua yaharibu nyumba zaidi ya 100 mkoani Rukwa

Picha ya mtandao
NYUMBA 160 zimeharibiwa na mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali zinazoendelea kunyesha wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa huku watu 1,200 wakikadiriwa kuathirika na kukosa makazi ya kudumu.

Nyumba hizo zimeharibiwa na mvua za masika zilizoambatana na upepo mkali zilizoanza kunyesha katika mkoa wa Rukwa kuanzia Septemba mwaka jana hadi mapema mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfani Haule, alisema kuwa tathmini ya awali iliyofanyika imebaini kuwa ujenzi wa chini ya viwango wa nyumba za makazi vijijini ni miongoni mwa sababu ya nyumba hizo zaidi ya 1,000 kubomolewa kwa mvua za masika na kuzisababishia familia nyingi hasara kubwa.

Aliitaja sababu nyingine ni uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo ukataji na uchamaji miti ovyo na kusababisha maeneo mengi vijijini yakibaki bila miti ambayo ingeweza kuzuia upepo mkali.

Alivitaja vijiji vilivyoathiriwa kwa mvua hizo za masika katika wilaya ya Sumbawanga kuwa ni Uzia kilichopo katika Bonde la Ziwa Rukwa ambapo familia kadhaa zimekosa makazi ya kudumu baada ya nyumba zao 64 kubomolea na mvua hizo. Watu 19 wamejeruhiwa.

Alisema katika tukio hilo nyumba 50 zimeharibika vibaya ambapo paa na kuta zimeanguka. Vjiji vingine ni Mtimbwa, manispaa ya Sumbawanga ambapo nyumba 27 ziliharibiwa, mbuzi nane, kuku zaidi ya 100 na nguruwe mmoja walikufa.

Kijiji cha Mwela katika Bonde la Ziwa Rukwa nyumba 23 ziliharibiwa na kujeruhi watoto wanne wa familia moja. Katika vijiji vya Mpwapwa na Jangwani nyumba 43 ziliharibiwa na kumjeruhi mtoto mmoja wa miaka sita huku zaidi ya watu 250 wakiwa wamekosa makazi ya kudumu.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mpwapwa , Marekani Kayembe ,alisema kuwa katika kijiji hicho nyumba 24 ziliezuliwa paa na kuanguka kuta na watu 120 hawana makazi ya kudumu.

Mkazi wa kijiji cha Jangwani, Bahati Mangula, alisema kuwa mvua hiyo ilisababisha taharuki kwa wakazi ambapo yeye na watoto wake wawili walisalimika kwani walikuwa wamejificha uvunguni mwa kitanda wakati ukuta wa nyumba yao ulipoanguka.

Diwani wa Mpwapwa, Abel Kambaulaya amewaomba wasamaria wema kutoa msaada wa hali na mali kwa waathirika hao ambao nyumba zao na vyakula vyao vimeharibiwa na mvua hiyo.

Dk Haule alisema tayari Serikali ya wilaya kupitia kamati yake ya maafa imeshatoa misaada ya mabati na mbao kwa walioathirika katika kijiji cha Mtimbwa huku katika kijiji cha Uzia waathirika ambao nyumba zao zipatazo 50 ziliharibiwa vibaya wamesaidiwa maturubali kwa ajili ya kujihifadhi kwa muda.

ZeroDegree.
Mvua yaharibu nyumba zaidi ya 100 mkoani Rukwa Mvua yaharibu nyumba zaidi ya 100 mkoani Rukwa Reviewed by Zero Degree on 1/13/2017 11:47:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.