Loading...

Mshahara wapanda kwa 100%

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein 
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amepandisha mishahara ya kima cha chini kwa asilimia 100 kutoka Sh150,000 hadi Sh300,000 kuanzia Aprili.

Dk Shein alitoa tamko hilo alipokuwa akihutubia katika sherehe za kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hiyo ni ahadi aliyoitoa Dk Shein wakati wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 na pia katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi, 2016.

Kabla ya tamko la Dk Shein jana, Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Dk Khalid Mohamed aliwahi kuwasilisha pia mapendekezo yake katika hotuba yake ya bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 ndani ya Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi mapema mwezi Julai mwaka jana kuhusu mishahara ya kima cha chini.

Akihutubia jana katika sherehe za maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja, Dk Shein alisema: “Maandalizi ya kuwalipa wafanyakazi wote wa kima cha chini cha mshahara wa Sh300,000 kutokea kiwango cha sasa cha Sh150,000 ifikapo mwezi wa Aprili mwaka huu tayari.”

Katika hotuba yake ya takribani saa moja na dakika 20, Dk Shein alizungumzia mafanikio ya serikali anayoiongoza na pia katika sekta za uchumi, siasa, huduma za kijamii, na suala la amani na utulivu.

Kauli za wananchi juu ya ahadi za Dk Shein


Baadhi ya wananchi wakiwamo wafanyakazi wa sekta mbalimbali za Serikali na binafsi walionekana kutoamini uamuzi huo, baadhi wakifurahia na wengine kusema wanasubiri kwanza waone mishahara mipya ikilipwa.

“Tungojee tuone hapo itakapofika mwezi Aprili, maana hii si mara ya kwanza kuyasikia haya,” alisema Hidaya Juma (45) mkazi wa Kianga mjini Unguja.

Kwa upande wake, Masoud Abdalla (54), ambaye ni mfanyakazi wa Wizara ya Ajira, Vijana, Wanawake na Watoto alisema: “Wenzetu wa manispaa sijui kama washaupata mshahara mpaka sasa, lakini ikibidi hivyo si haba. Tutakuwa tumepata la maana.”

Chum Simai (43) mkazi wa Jang’ombe aliyedai ni mlinzi katika moja ya ofisi za Serikali alisema haamini hadi atakapopata mshahara mpya.

Akizungumzia kupanda kwa mishahara kwa kiwango hicho, naibu katibu mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Jones Majura alisema uamuzi wa Dk Shein utawafanya nao wao wapeleke mapendekezo serikalini ili mshahara wa kima cha chini upande.

Mbali na kuzungumzia suala la mishahara, Dk Shein alieleza mwenendo wa biashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kuwa iliimarika kwa kiasi kubwa ambapo kiasi cha bidhaa za Sh 53.13 bilioni ziliagizwa kutoka Bara kwenda Zanzibar sambamba na zile za Sh 118 bilioni kutoka Zanzibar kuelekea Bara.

Alisema kuwa uimarishaji wa sekta ya biashara ulikuwa na ongezeko la asilimia saba, akisema kwa mwaka 2016 Zanzibar iliagiza bidhaa za thamani ya Sh167 bilioni tofauti na mwaka 2015 ilipoagiza kiasi ya bidhaa za Sh156 bilioni.

Dk Shein alipongeza juhudi za kuimarisha sekta ya uchumi kwa kutumia wawekezaji wazalendo ambao ni pamoja na Viwanda vya Maziwa vya Fumba, hoteli ya hadhi ya nyota tano ya Mtoni Marine na kiwanda cha Mtoni Milling, vinavyomilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Salim Said Bakhressa na viwanda vya sukari vya Mahonda na cha matrekta cha Mbweni.

Huduma za kijamii, miundombinu


Dk Shein pia alisema serikali yake ilifanya juhudi za kuimarisha huduma za kijamii za elimu, afya, maji, utalii na miundombinu tangu alipochaguliwa tena Machi mwaka huu kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Alitoa mfano wa barabara ya kilomita nne ya kutoka Mwanakwerekwe hadi Fuoni inayojengwa kwa kiwango cha lami, sambamba na nyingine zinazoendelea kujengwa katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisifu juhudi zilizochukuliwa na serikali yake katika mwaka uliopita, akisema walifanikiwa kununua meli mpya ya abiria ya Mv Mapinduzi II na kuimarisha ufanisi katika Bandari ya Malindi kwa kununua vifaa vya kisasa, sambamba na azma iliyopo ya kununua meli nyingine mpya ndogo kwa ajili ya abiria, mizigo na mafuta.

Kuhusu nishati, Dk Shein alisema pamoja na Zanzibar kupitisha Sheria Na 6 ya Mwaka 2016 ya Utafutaji na Uchimbaji Mafuta na Gesi, alimshukuru Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ambaye alisema aliweka mazingira ya kufanikisha azma hiyo. Alisema huduma ya umeme iliimarishwa kwa kuwaungia umeme kwa njia ya mkopo zaidi ya wananchi 4,487 wa Unguja na Pemba.

Matukio yasiyo ya kawaida 

Umati uliokusanyika kwenye Uwanja wa Amaan kushuhudia kilele hicho cha maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi, haukuweza kumuona Rais John Magufuli, ikiwa ni tukio la nadra kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kutohudhuria sherehe hizo.

Rais alishasema si lazima watu wote warundikane sehemu moja wakati wa sherehe za kitaifa na badala yake watawanyike nchi nzima, na Magufuli jana aliongoza sherehe kama hizo mkoani Shinyanga, akiwa pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.

Dk Shein aliutangazia umma kuwa Dk Magufuli aliwasiliana naye kumuhakikishia kuendelea kwa ushirikiano baina ya pande mbili licha ya mkuu huyo wa nchi kukabiliwa na ziara muhimu pamoja na mkutano wa hadhara mkoani Shinyanga jana.

Wahudhuriaji walitarajia utamaduni wa kiongozi mkuu wa nchi kuwepo. “Tulitarajia kumuona hapa kazi tu (kaulimbiu ya Rais Magufuli) akiwepo Amaan. Mambo yangelikuwa mazuri zaidi lakini ametuangusha kidogo,” alisema mmoja wa wahudhuriaji wa sherehe hizo, Abdalla Said (27) mkazi wa Saateni.

Lakini mkazi mwingine wa Kihinani kisiwani hapa, Kassim Shomari alisema ni vyema kwa viongozi wa kitaifa kujiandaa kwa sherehe za kitaifa.

“Viongozi lazima wajipange vyema pamoja na ratiba zao maana mtu kama yule kukosekana hapa haileti picha nzuri,” alisema Shomari (46).

Lakini Msimu Ali (25), ambaye ni mkazi wa Fuoni, alisema alichokosa ni burudani kutoka kwa mkuu huyo wa nchi.

“Leo tumekosa raha za mzee wa hapa kazi tu, hayupo,” alisema.

Viongozi waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Majaji Wakuu Othman Chande na Omar Makungu wa Zanzibar, marais wastaafu wa Zanzibar na wale wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mawaziri wakuu wastaafu, mawaziri, wabunge, wajumbe wa Baraza la Wakilishi, viongozi, watendaji wa Serikali zote na wananchi wa mikoa yote mitano ya Unguja na Pemba.

Suala jingine ambalo si la kawaida na ambalo huenda lilitokana na Rais Magufuli kutohudhuria sherehe hizo, ni kitendo cha Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange kwenda kupokea heshima ya vikosi vya ulinzi na usalama mara tu alipofika uwanjani.

Baada ya kushuka kwenye gari, Jenerali Mwamunyange alikwenda moja kwa moja kwenye kibanda kilichowekwa mbele ya vikosi hivyo na kutambulishwa na baadaye kupigiwa saluti kabla ya kwenda jukwaani.

Kwa kawaida heshima hiyo hupewa Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye ni amiri jeshi mkuu wa vikosi vikosi vya ulinzi na usalama.

Katika tukio jingine, sherehe za Mapinduzi mwaka huu zimefanyika kwa wakati mmoja sehemu mbili tofauti, yaani Bara na Visiwani tofauti na miaka iliyopita.

Akizungumza kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga kabla ya Rais kuhutubia, Waziri wa Nchi (Tamisemi, Kitengo Maalum), Haji Omari Kheir alisema hii ni mara ya kwanza kwa sikukuu hiyo kuadhimishwa sehemu mbili za Muungano.

Alisema kufanyika sehemu mbili tofauti za Muungano ni tukio la kihistoria.

Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Mshahara wapanda kwa 100% Mshahara wapanda kwa 100% Reviewed by Zero Degree on 1/13/2017 11:55:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.