Loading...

Serikali kupeleka umeme katika vijiji 8,000 nchini

MRADI Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), utaanza rasmi kutekelezwa mwezi ujao, imefahamika.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo mjini Dodoma wakati akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, waliokutana na watendaji wa wizara hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, Profesa Muhongo ameongeza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, serikali imepanga kuwakabidhi makandarasi watakaotekeleza mradi huo kwa wabunge ili kuhakikisha kwamba mradi husika unatekelezwa kikamilifu.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/17 bungeni mwaka jana, Profesa Muhongo alisema serikali itafanya tathimini ya kina ya awamu ya kwanza na ya pili ya kupeleka umeme vijijini, lengo likiwa ni kuboresha maandalizi ya utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi huo.

Alisema pamoja na tathimini hiyo, masuala yatakayozingatiwa katika awamu ya tatu ni kupeleka umeme kwenye vijiji ambavyo havikupata umeme katika awamu ya kwanza na ya pili; kwenye viwanda vidogo vya uzalishaji mali; na katika shule za sekondari, hospitali, zahanati, vituo vya afya, pampu za maji na maeneo mengine muhimu ya huduma za kijamii.

Alisema awamu hiyo ya tatu, itaanza katika mwaka 2016/17 na kukamilika mwaka 2018/19.

Vijiji 8,000 vinatarajiwa kupatiwa umeme chini ya mradi wa REA Awamu ya Tatu. Wakati huo huo, Kamati hiyo ya Bunge kupitia kwa Mwenyekiti wake, Dotto Biteko imeipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa ukusanyaji wa maduhuli kwa kipindi cha nusu mwaka na kueleza kuwa mwelekeo wa ukusanyaji huo, unakwenda vizuri.

Awali, akiwasilisha taarifa ya wizara kuhusu upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha nusu mwaka kwa Kamati, Katibu Mkuu wa wizara, Profesa Justin Ntalikwa alieleza kuwa hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana, wizara ilikuwa imekusanya jumla ya Sh bilioni 201.86 sawa na asilimia 54.46 ya lengo lililokusudiwa.

“Mapato hayo yanatokana na vyanzo mbalimbali vikiwemo ada za kijiolojia, mrahaba, ada za mwaka za leseni, mauzo ya nyaraka za zabuni, mauzo ya gesi asilia, tozo ya mauzo ya umeme na shughuli za utafiti wa mafuta na gesi asilia,” alieleza Profesa Ntalikwa.

Akieleza utekelezaji wa majukumu ya wizara kwa kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana, Katibu Mkuu alisema serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati kulingana na mpango wake na kuitaja miradi kadhaa ikiwemo Mradi wa Kusafirisha Umeme Msongo wa kilovoti 400 kutoka iringa hadi Shinyanga uliokamilika Desemba 28, 2016.

“Mradi wa Kinyerezi II wenye Megawati 240 utekelezaji wake umefikia asilimia 29 na Serikali imekwishatoa mchango wake wote wa asilimia 15 sawa na shilingi bilioni 110 na mradi huu unategemewa kukamilika mwaka 2018,” alisisitiza Profesa Ntalikwa.

Akizungumzia Mradi wa Kinyerezi I, Extension ya Megawati 185 ambao ni mwendelezo wa upanuzi wa Mradi wa Kinyerezi 1, ameeleza kuwa, mradi huo unaendelea kutekelezwa na unatarajiwa kukamilika mwaka 2018.

Akizungumzia uendelezaji wa uchimbaji mdogo, Profesa Ntalikwa alisema ili kukuza utendaji wao, wizara inaendelea na hatua za uanzishwaji wa vituo vya mfano vitano katika wilaya za Kilwa, Mpanda, Chunya na Bukoba kwa ajili ya wachimbaji wadogo; ambavyo vitatumiwa na wachimbaji hao kuchenjua madini yao na kujifunza namna bora ya kuendesha migodi yao kitaalamu na kwa tija zaidi.

Ahadi ya Waziri Mkuu Akizungumza na watendaji wa idara za serikali wilayani Longido katika ziara yake ya kikazi mkoani Arusha Desemba mwaka jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema serikali imesaini mkataba kwa ajili ya kukamilisha kuweka umeme katika vijiji 8,000 vilivyosalia katika awamu ya kwanza na ya pili ya Mradi wa Umeme Vijijini (REA).

Alisema wakandarasi walishasaini mikataba hiyo na kwamba mwezi Aprili 2017, vijiji hivyo vitakuwa vimeshapata umeme.

Alisema maeneo ambayo umeme huo hautafika, wananchi watafungiwa nishati ya umeme wa jua kwa gharama ile ile ya Sh 27,000, ambayo ni sawa na gharama za umeme wa gridi ya taifa. Waziri Mkuu alisema baada ya miradi hiyo kukamilika, vijiji vyote nchini vitakuwa na umeme.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, umeme huo utawezesha wananchi kujikwamua na hali ngumu ya maisha kwa kubuni miradi mbalimbali ya uzalishaji mali katika maeneo yao.

Muhongo akiwa Mara Kwa upande wake, Profesa Muhongo alisema vijiji vyote ambavyo havijafikishiwa huduma ya umeme, vitapata huduma hiyo kupitia mradi mkubwa wa umeme vijijini Awamu ya Tatu unaotekelezwa na REA.

Alisema hayo katika ziara yake mkoani Mara mwaka jana, kukagua utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini Awamu ya Pili (REA II) ambao unamalizika.

Alisema katika maeneo mbalimbali aliyotembelea, alielezwa kuwa vijiji vya ndani, havina umeme kwani nishati hiyo imeishia kwenye vijiji vilivyopo katika barabara kubwa na kwenye vituo vya biashara. Alisema serikali inatambua vijiji ambavyo havikufikishiwa huduma hiyo, hivyo aliwaomba wananchi katika vijiji hivyo kuwa na subira.

Alisema mradi wa REA III umetengewa zaidi ya Sh trilioni moja, ambayo ni mara tatu zaidi ya iliyotengwa katika mradi wa REA II ambao unamalizika kwa kuunganisha baadhi ya vijiji.

ZeroDegree.
Serikali kupeleka umeme katika vijiji 8,000 nchini Serikali kupeleka umeme katika vijiji 8,000 nchini Reviewed by Zero Degree on 1/25/2017 10:21:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.