Loading...

9 yanayoweza kutokea kwenye mechi ya Simba na Yanga Jumamosi Tarehe 25, Februari 2017

TAYARI vijembe na kejeli zimeanza mitaani kuelekea mchezo huu huku kila upande ukijinasibu kuibuka na ushindi siku hiyo kisa ubora wa kikosi chao.

Kuna baadhi ya mambo yamekuwa kama desturi sasa kwenye mechi za Simba na Yanga, karibu kila mchezo yamekuwa yakijirudia.

Watani wa jadi Simba na Yanga watavaana siku ya Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu, mechi inayotarajiwa kupigwa majira ya saa kumi jioni uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Haya hapa mambo 9 yanayotarajiwa kutokea kwenye mchezo huo:

  1. Mfumo wa kielotroniki kuchelewesha mashabiki kuingia kiwanjani
    Msimu huu TFF wamekuwa wakitumia mfumo wa kisasa wa kieletroniki kuingia kiwanjani hasa kwenye kiwanja cha Taifa na kile cha Uhuru, ila mfumo huu umekuwa na changamoto nyingi ikiwemo kusimama kufanya kazi kwa baadhi ya mashine kutokana na kuzidiwa na idadi ya mashabiki, hivyo mchezo wa Jumamosi kuna uwezekano wa mashine hizi kuchelewesha watu kuingia kiwanjani kutokana na idadi ya watu siku hiyo huku mashine zikiwa chache.
  2. Mashabiki wa kila upande kuzimia
    Imekuwa kama desturi kwenye mechi za Watani wa jadi kuona kundi kubwa la mashabiki wakidondoka kutokana na presha ya timu yao kufungwa na hata wakati mwingine husababishwa na ushindi, bila shaka hata wikendi hii hali ya mashabiki kudondoka bado itaendelea
  3. Simba kumiliki mpira kwa muda mwingi wa mchezo
    Katika michezo ya hivi karibuni kati ya Simba na Yanga, Wekundu wa Msimbazi wamekuwa wakitawala katikati kwa muda mwingi wa mchezo, wana wachezaji wa kati wenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira kwa asilimia kubwa au inawezekana ikawa pia ni mbinu za makocha wa pande mbili.

    Kwamba, inawezekana makocha wa Simba wanapenda timu imiliki mpira na kutengeneza nafasi kwa kutokea eneo la katikati au pembeni lakini inawezekana Yanga wao huamua kuwaacha Simba wamiliki mpira halafu wao wakiupata wanafanya mashambulizi ya kushtukiza.
  4. Tambwe kuifunga Simba kwenye mchezo huo

    Mrundi huyu amekuwa kwenye wakati mzuri pindi achezapo na Simba, kuwafunga kwake imekuwa kitu cha kawaida hata siku hiyo wasipo mwekea ulinzi thabiti bado mshambuliaji huyu atawaadhibu
  5. Lawama zote kwa mwamuzi kwa timu itakayofungwa
    Mwamuzi wa mchezo huo lazima ataangushiwa zigo la lawama kutoka kwa timu itakayo poteza mechi, klabu hizi zimekuwa zikificha udhaifu wao kwa kumwangushia refa mzigo wa lawama kwamba kawaonea au refa kaibeba timu fulani na hakuna timu ambayo hukubali kwamba imepoteza mchezo kutokana na ubora wa mpinzani wao.
  6. Imani za kishirikina
    Mchezo huo unakabiliwa na imani za kishirikina kwa timu hizo kwa kwenda uwanjani kufukia vitu kabla ya mechi au kukataa kupita katika milango ya kuingilia iliyozoeleka kwa kudhani wamewekewa vitu au wakati mwingine kugoma kuingia vyumbani kwa kuhofia vyumba huenda vimepuliziwa dawa za kuwamaliza nguvu.
  7. Vurugu za Mashabiki Uwanjani
    Tulishuhudia mchezo uliopita Mashabiki wa Simba waling’oa viti, baada ya kutoridhishwa na maamuzi ya Martin Sanya ambae ndiyo alikua refa katika mtanange huo.
  8. Lawama kwa Makocha na viongozi
    Tumekuwa tukiona vilabu hivi viwili vikitimua makocha iwapo kocha mmoja wapo atafungwa na mpinzani wake katika “derby” hiyo ambayo imesababisha vibarua vya makocha wengi kufikia baada ya timu kupoteza mechi dhidi ya watani zao.
  9. Ulinzi

    Katika mtanange huo kutakuwa na ulinzi mkali kuanzia nje ya uwanja hadi ndani hivyo kutakuwa na ukaguzi mkali katika milango yote ili kuhakikisha wanaoingia uwanjani wote hawana vitu vyenye uwezekano wa kuleta madhara kwa watazamaji wengine.
Source: ShaffihDauda
9 yanayoweza kutokea kwenye mechi ya Simba na Yanga Jumamosi Tarehe 25, Februari 2017 9 yanayoweza kutokea kwenye mechi ya Simba na Yanga Jumamosi Tarehe 25, Februari 2017 Reviewed by Zero Degree on 2/23/2017 01:47:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.