Loading...

Baraza la viongozi wa dini laomba RC Makonda aongezewe ulinzi wa kutosha

BARAZA la Viongozi wa Dini la Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, limeiomba mamlaka inayohusika kumwongezea ulinzi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutokana na vita vyake vya mihadarati alivyoanzisha.

Viongozi hao mbali na kumpongeza Makonda, wamesema vita hivyo vinahitaji ulinzi wa kutosha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema jitihada zinazoendelea dhidi ya dawa za kulevya ni mkakati wa kuokoa nguvukazi ya taifa.

“Tunampongeza kwa dhati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa ujasiri mkubwa aliouonyesha kwa kuwa ameamua kujitoa muhanga kwa ajili ya taifa lake na watu wake na pia ameonyesha uthubutu,” alisema.

Alisema baraza hilo lipo chini ya Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania na wamekuwa wakipiga vita na kulaani vitendo vya kushamiri kwa biashara au utumiaji wa dawa za kulevya.

Sheikh Salum alisema matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo katika nchi na kupoteza nguvukazi ya taifa kwa kuwa waathirika wakubwa wa matumizi ya dawa hizo ni vijana.

“Licha ya kumpongeza, pia tunapenda kumhakikishia kuwa tunaunga mkono juhudi zake alizozianza na kwamba tupo pamoja naye," alisema.

"Kutokana na ugumu wa kazi hii tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu ili ampe ulinzi na azidi kuwa na moyo wa ujasiri wa kupambana na maovu yote yanayoharibu sifa la taifa na vijana wetu.”

Aidha, Sheikh Salum alisema ambao wanapinga na kubeza juhudi hizo ni ambao hawajawahi kuguswa na madhara ya dawa za kulevya katika familia zao.

Alisema watu kama hao hawana uchungu na Watanzania wenzao walioathirika.

Pia Baraza hilo limewaomba viongozi wengine kuiga mfano kutoka kwa Makonda katika kupambana na uovu huo kwani ni janga la taifa na Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana.

Aidha, amewaomba wananchi kuunga mkono jitihada hizo kwa kutoa ushirikiano na vyombo husika ili kutokomeza dawa za kulevya nchini.
Baraza la viongozi wa dini laomba RC Makonda aongezewe ulinzi wa kutosha Baraza la viongozi wa dini laomba RC Makonda aongezewe ulinzi wa kutosha Reviewed by Zero Degree on 2/10/2017 11:10:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.