Loading...

Jukwaa la katiba [JUKATA] latoa neno juu ya ukimya katika mchakato wa uundwaji katiba mpya

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba 
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba amesema kuna hali ya sintofahamu kuhusiana na mchakato wa Katiba Mpya kutokana kutotolewa kwa taarifa yoyote ya kinachoendelea.

Kibamba amesema hayo mbele ya wanahabari mjini Dar es Salaam kwamba, ukimya huo unawatia hofu iwapo suala hilo litashughulikiwa ama la.

“Wananchi wengi walitegemea Serikali ingeweza kutoa mwelekeo wa mchakato wa Katiba Mpya, lakini sasa ni mwaka mmoja umepita hakuna kinachoendelea,” amesema Kibamba.

Ameongeza kuwa muda wa kukamilisha upatikanaji wa Katiba Mpya ni mwaka 2017/18, kipindi hicho kisipotumika kukamilisha mchakato kuna uwezekano ikaja kupatikana mwaka 2020.

“Kwa sababu mwaka 2019 ni wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baada ya hapo joto la Uchaguzi Mkuu wa 2020 litakuwa juu hakutakuwa na mchakato tena,” amesema Kibamba.

Awali, ametoa rai kwa viongozi wa Serikali waliokasimishwa madaraka kufanya kazi zao kwa kufuata sheria, kanuni na utaratibu wa utumishi wa umma kama walivyoapa.

Rai hiyo imekuja siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutaja majina ya wanaodaiwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya na kuwataka wafike Kituo Kikuu cha Polisi mkoani humo kwa ajili ya mahojiano.

Naye Mkurugenzi wa Jukata, Hebron Mwakagenda amesema kuna haja kwa vyombo vya kutoa haki navyo visimame kupinga yale yanayoiangamiza nchi.

Source: Mwananchi
Jukwaa la katiba [JUKATA] latoa neno juu ya ukimya katika mchakato wa uundwaji katiba mpya Jukwaa la katiba [JUKATA] latoa neno juu ya ukimya katika mchakato wa uundwaji katiba mpya Reviewed by Zero Degree on 2/12/2017 10:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.