Loading...

Mikataba mipya ya Donald Ngoma na Vincent Bossou ni kufuru

Hadi kufikia leo Februari mosi, wachezaji wageni wa Yanga, Ngoma, Bossou, Thaban Kamusoko na Amis Tambwe watakuwa wamebakiza miezi minne tu kabla ya kumaliza mikataba yao, huku wenzao wa ‘Kibongo’ Matteo Anthony, Malimi Busungu na Deus Kaseke pia mikataba yao itakuwa imemalizika kufikia mwishoni mwa msimu huu wa ligi.

Kikanuni wachezaji hao wanaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu yoyote mpya kwa ajili ya msimu ujao, huku wakiendelea kumalizia miezi yao minne iliyosalia au kama wakiamua kuinunua. Lakini pia wanaweza kuongeza mikataba ili kuendelea kuitumikia klabu hiyo ya mitaa ya Jangwani na Twiga.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alisema suala la wachezaji hao lipo mikononi mwa Kamati ya Usajili ambapo walishaanza mazungumzo nao lakini yalisitishwa baada ya wachezaji, Bossou na Ngoma kuondoka nchini.



Sanga alisema tayari Ngoma amewasili jana asubuhi na Bossou alitarajiwa kuwasili jana jioni, ambapo anaamini kuwa mazungumzo baina yao na Kamati ya Usajili yataendelea vizuri na kufikia mwafaka.

“Ni kweli Ngoma na Bossou mikataba yao ipo ukingoni, lakini tayari suala lao linashughulikiwa na Kamati ya Usajili na walishaanza mazungumzo nao na kila kitu kitakwenda sawa,” alisema.

DIMBA lilikwenda mbali zaidi na kumtafuta mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, Abdallah Bin Kleb ambaye hata hivyo hakuwa tayari kuweka wazi juu ya jambo hilo.

Wachezaji hao kila mmoja aliondoka kwenda nchini kwake kutokana na sababu tofauti, ambapo Bossou alikwenda kujiunga na timu yake ya Taifa ya Togo iliyokuwa inashiriki michuano ya Afcon, huku Ngoma akielekea kwao Zimbabwe kwa ajili ya kuhudhuria msiba wa kaka yake mkubwa, ingawa na yeye mwenyewe ni majeruhi tangu walipotoka kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi kisiwani Zanzibar.

Yanga na Simba zimekuwa na changamoto kubwa ya wachezaji wake kufikia mwishoni mwa mikataba yao ambapo kwa Simba, nyota muhimu kama Jonas Mkude, Juuko Murshid na Ibrahim Ajib, pia wanaelekea ukingoni mwa mikataba yao lakini tayari vigogo wa klabu hiyo ya Msimbazi wameahidi kuwapatia mikataba mipya wachezaji hao.

Source: Dimba
Mikataba mipya ya Donald Ngoma na Vincent Bossou ni kufuru Mikataba mipya ya Donald Ngoma na Vincent Bossou ni kufuru Reviewed by Zero Degree on 2/01/2017 02:07:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.