Loading...

Tathmini ya ushindani uliopo katika La Liga na msimamo wa ligi hiyo mpaka sasa

MPAKA sasa ni ngumu sana kutabiri ni nani atabeba taji msimu huu kwenye La Liga nchini Hispania na hii ni kwa sababu ya ushindani unaoonyeshwa na klabu kubwa katika msimamo.

Vinara wa ligi, Real Madrid, walianza vyema msimu na kufanya wengi waamini kuwa huu ni mwaka wao wa kumaliza mkosi wa kulikosa taji hilo kwa msimu zaidi ya mitatu sasa.

Lakini ghafla wakapoteza dira na kuonekana kama wamekata pumzi, wakadondosha pointi muhimu katikati ya safari.

Vichapo hivyo vikawapelekea kupoteza rekodi yao ya kucheza michezo 39 bila kufungwa, huku Sevilla, klabu iliyo kwenye kiwango bora msimu huu ikitoa kichapo cha kuvunja mwiko huo.

Siku chache baadaye, wakatandikwa tena na Celta Vigo na kuondoshwa kwenye Copa del Rey.

Vichapo hivi vya ghafla, vikapelekea kuibuka kwa maswali mengi kwa kocha Zinedine Zidane. Ni vipi angeweza kurudi na kuendeleza moto wa Madrid?

Ndio, Zidane alitulia na kuirejesha Real kwenye mstari kwa kuichapa bila huruma Real Sociedad kwa bao 3-0.

Mpaka sasa Real ndio timu iliyofunga mabao mengi msimu huu (mabao 51) na wana faida ya mchezo mmoja mkononi hivyo kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuendeleza kasi yao na kutwaa ubingwa.

Msimamo wa La Liga:


Kwa Barcelona wanaoshika nafasi ya pili, sare ya bao 1-1 waliyoipata ugenini dhidi ya Real Betis inaweza kuwa ni ishara ya mwisho wa ndoa yao na kocha Luis Enrique.

Kisa nini? Kwanza Barcelona ndio timu pekee kati ya tatu zilizo juu kwenye msimamo iliyofanya makosa mengi kwenye lango lao na kupelekea wapinzani kutikisa nyavu zao.

Kwa mtazamo huu ni wazi kuwa kuna tatizo la kiufundi ndani ya Barcelona na Enrique ndio anayetakiwa kuwajibika nalo.

Kwa Atletico Madrid, wao bado wanaendelea kushikilia rekodi ya kuwa timu yenye ukuta mgumu japo msimu huu wanaonekana si imara kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Kuyumba kwao kunatokana na safu ya ushambuliaji kuboronga na kushindwa kupachika mabao hali inayoonekana kuiweka rehani nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa msimu ujao.

Unajua kwanini? Sevilla chini ya kocha Jorge Sampaoli, imekuwa timu bora msimu huu ikicheza soka la kuvutia kwa dakika zote wanazokuwa uwanjani.

Japo kumekuwa na matukio mengi ya kushtua msimu huu, kama klabu iliyopanda daraja, Alaves kuichapa Barcelona.

Wachovu wengine, Leganes kuikomalia Atletico kwenye mchezo wao wa kwanza kabisa ndani ya La Liga lakini bado uwezo wa Sevilla msimu huu umeendelea kushtua wapenzi wengi wa soka la nchini Hispania.

Wanacheza soka la kasi na mshikamo hivyo si ajabu ukiwaona kwenye nafasi ya tatu wakilingana pointi na Barcelona wanaoshika nafasi ya pili. Atletico Madrid wako kwenye nafasi ya nne na wanaendelea kufukuza mwizi kimya kimya.

Ukiachana na uwezo wa timu, ziko takwimu binafsi za wachezaji zinazoonekana kuteka hisia za wengi mpaka wakati huu.

Kiungo wa Real Madrid, Mjerumani Toni Kroos, anaongoza kwa asisti msimu huu, akitoa asisti 9 na kuwa sehemu ya mchango mkubwa wa vinara hao wa ligi.

Katika suala zima la kukokota mipira, si ajabu ukiyakuta majina ya nyota wawili wa Barcelona, Neymar na Lionel Messi, japo kinda wa Celta Vigo, Theo Bongonda ameonyesha kuwa na ubunifu mkubwa wa kukokota mipira.

Bila shaka ukiambiwa utaje wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Sevilla, jina la kiungo Steven N’Zonzi huwezi kuacha kulitaja. Huyu ndiye kinara wa kupiga pasi nyingi msimu huu.

Tukija katika suala zima la ufungaji, Luis Suarez anaongoza akiwa na mabao 16, akifuatiwa kwa karibu na mshindi mara tano wa Ballon d’Or, Lionel Messi, mwenye mabao 16.

Nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo anayeonekana kuporomoka kiwango msimu huu, anakatamata nafasi ya tatu akiwa na mabao 13.

Mbali na hilo, tayari kura zimeshaanza kupigwa katika kupendekeza lipi linafaa kuwa bao bora la msimu, mengi yametajwa likiwamo lile la Raul Garcia wa Athletic Bilbao alilofunga dhidi ya Deportivo La Coruna, Septemba mwaka jana.

Kevin-Prince Boateng naye yuko kwenye orodha hii sambamba na straika wa Atletic Madrid, anayewindwa vikali na mashetani wekundu wa Old Trafford, Antoine Griezmann.
Tathmini ya ushindani uliopo katika La Liga na msimamo wa ligi hiyo mpaka sasa Tathmini ya ushindani uliopo katika La Liga na msimamo wa ligi hiyo mpaka sasa Reviewed by Zero Degree on 2/04/2017 01:58:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.