Loading...

Kilio cha ukata wa fedha chafika hadi kwa CAG

Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad.
OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), imesema hadi sasa haijapewa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali, hali inayosababisha mipango mingi kukwama.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa ofisi hiyo jana mjini hapa, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad, alisema ofisi yake huhitaji Sh. bilioni 10 kwa ajili ya uendeshaji, lakini hadi sasa haijapata licha ya kupeleka maombi serikalini.

Akifafanua matumizi ya fedha hizo katika ofisi hiyo inayoshughulika na masuala ya ukaguzi wa fedha za serikali, CAG alisema huhitaji Sh. bilioni nane kwa matumizi ya kawaida ya kila mwaka, ikiwamo kuwapeleka kwenye mafunzo ya ukaguzi ya kimataifa wakaguzi wa hapa nchini.

“Hadi sasa bado hatujapewa fedha hizo ambazo zingeweza kutusaidia katika kazi zetu za kila siku na hali hii imesababisha shughuli mbalimbali kulala,” alisema Prof. Assad.

Kutokana na hali hiyo, CAG aliiomba Wizara ya Fedha na Mipango kusaidia ili kuendelea na mikakati ya bajeti ya mwaka 2016/2017.

Prof. Assad alisema kutopatikana kwa fedha hizo pia kumesababisha ofisi yake kushindwa kuendelea na ujenzi wa ofisi zake katika mikoa mbalimbali, ukiwamo Rukwa, jambo ambalo linawapa shida.

Alibainisha pia ofisi yake imeshindwa hata kupeleka wakaguzi katika mafunzo ya ukaguzi wa kimataifa, kutokana na kukabiliwa na ukata huo.

“Tumeshindwa kupeleka wakaguzi katika mafunzo ya kimataifa na jambo hili si zuri hata kidogo.Lakini sina jinsi, inabidi kukubali tu,” alisema Prof. Assad.

Alisema kama wakaguzi wataendelezwa kimataifa, itasaidia nchi kuepuka kudanganywa kila kukicha kwa kuwa watakuwa na wakaguzi wa kimataifa kutoka hapa nchini.

Aliiomba serikali kuwapatia kiasi hicho walau kwa awamu ili waweze kuanza kugharamia vitu vingine ambavyo vina uhitaji wa haraka wakati wakisubiri bajeti nzima.

“Tunaomba serikali katika bajeti zetu za mwaka waongeze ili isaidie kupunguza kero ambazo zinatukabili katika mipango mikakati ya kuboresha kazi za kila siku,” alisema.

WAKAGUZI 10

Akizungumzia ujenzi wa Chuo cha Ukaguzi cha Gezaulole, Prof. Assad alisema walipata wafadhili kwa ajili ya kuwasaidia, lakini wanashindwa kuwaleta kutokana na ukata unaoendelea kuwakabili.

“Tunaiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha itusaidie fedha hizo, tunahitaji kuendeleza wakaguzi, pamoja na ujenzi wa chuo hicho. Hadi sasa kuna wakaguzi 10 wameshindwa kwenda katika ukaguzi wa Halmashauri, kwa sababu hatuna fedha,” alisema.

Akifungua baraza hilo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Khatib Kazungu, alisema pamoja na changamoto zote zinazoikabili ofisi hiyo, ni lazima ifanye kazi kwa weledi zaidi kwa sababu sekta ya hesabu ni muhimu.

Alisema wakaguzi wanatakiwa kuwa waadilifu kuliko hata yule anayemkagua.

“Natambua ufinyu wa bajeti na ucheleweshaji wa mgawo unavyoathiri utendaji wenu wa kazi za ukaguzi,"alisema. Kazungu ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, James Dotto na kuongeza kuwa: "Nitawasilisha ombi hili ili kuhakikisha ofisi yenu inapata fedha."

Alisema hali ni mbaya kifedha kwa sababu zaidi ya asilimia 30 ya makusanyo ya serikali kwa sasa yanatumika kulipa madeni, hivyo kuathiri bajeti kwa kiasi kikubwa.

Fungu la Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi lilikuwa miongoni mwa manne yaliyoibua mjadala mzito bungeni wakati wa vikao vya Bunge la Bajeti mjini Dodoma Mei mwaka jana baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kubaini kuwa kiwango cha fedha kilichopangwa kwa ajili ya Ofisi hiyo kilikuwa pungufu kwa asilimia 60 kulinganisha na makadirio ya matumizi kwa mwaka huu wa fedha.

Mafungu mengine yaliyolalamikiwa kwa kiasi kikubwa na wabunge Mfuko wa Bunge, Mahakama na Maji.

Wakati wa mjadala wa makadirio ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka huu wa fedha, Naibu Waziri Kivuli wa wizara hiyo, David Silinde, aliliambia Bunge kuwa upinzani ulibainika kuwa bajeti ya Ofisi ya CAG kwa mwaka 2016/17, imefyekwa kwa asilimia 60, ikilinganishwa na makadirio ya ofisi hiyo.

Alisema ofisi hiyo nyeti iliomba kuidhinishiwa Sh. bilioni 68.839 ili itekeleze majukumu yake, lakini serikali ilitenga Sh. bilioni 32.3. Kati ya fedha hizo zilizotengwa na serikali, Sh. bilioni 28.3 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida wakati Sh. bilioni nne ni za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hivi karibuni, CAG aliagizwa kufanya uchunguzi wa Sh. bilioni 440 zilizowekwa na Mamlaka ya Usimamizi Bandari (TPA) katika benki mbalimbali kwenye akaunti maalum, kutokana na kiasi kidogo cha riba kilicholipwa.

Agizo hilo lilitolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) bungeni. Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Hilaly, alisema akaunti hizo zilifunguliwa kwenye benki za CRDB, Standard Chartered, NMB na NBC.

Makamu Mwenyekiti huyo aliagiza CAG ashirikiane na Benki Kuu (BoT) na Kitengo cha Uchunguzi wa Fedha (FIU) katika uchunguzi huo.

Maagizo hayo ya kamati hiyo yalitokana na hoja za ukaguzi za CAG kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

CAG aliagizwa katika ukaguzi ujao wa TPA aangalie riba waliyokubaliana na faida iliyopatikana baada ya kuweka fedha Sh. bilioni 440 katika akaunti mbalimbali.
Kilio cha ukata wa fedha chafika hadi kwa CAG Kilio cha ukata wa fedha chafika hadi kwa CAG Reviewed by Zero Degree on 3/15/2017 12:55:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.