Loading...

Mashabiki Simba wamgeukia Joseph Omog

SIKU moja baada ya Simba kukwama kusonga mbele baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Mbeya City, mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salam, lawama zimemwangukia Kocha wa timu hiyo, Joseph Omog.

Omog ambaye ameiwezesha Simba kupata pointi 55 baada ya kucheza mechi 24, amelaumiwa kutokana na masuala mbalimbali ambayo mashabiki na wanachama wa Simba wamekuwa wakiyaona katika mechi mbalimbali za timu hiyo.

Habari za ndani kutoka Simba zinasema kuwa, Omog analalamikiwa na kitendo chake cha kushindwa kufanya uteuzi sahahi wa kikosi kwenye mchezo huo ambao ulikuwa muhimu sana katika kusafisha njia ya ubingwa kwa timu hiyo.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba kinaeleza kuwa, kocha huyo amekuwa mbishi na mara kadhaa anafanya uamuzi ambao umekuwa na athari sana kwa timu.

“Suala la kupanga kikosi ni kocha, kweli haingiliwi lakini kutokana na mazingira lazima kocha akubali kupata ushauri, mfano katika mechi ya jana upangaji wa kikosi ulionekana kuigharimu timu na tulizidiwa sana kwa kweli,” alisema mtoa habari wetu.

Alisema kocha wa Mbeya City, Kinnah Phiri, alithibitisha kuwa benchi la ufundi analoliongoza ni bora zaidi ya lile la Simba baada ya kuonyesha uwezo mkubwa kiufundi.

“Omog aliwaanzisha Jonas Mkude na Said Ndemla kwenye eneo la kiungo lakini walionekana kushindwa kuhimili mikiki mikiki na kusababisha kupwaya kwenye eneo hilo, lakini pia kwanini James Kotei alimchezesha beki wakati Juuko Murshid akiwa nje tena timu ikiwa ina mapungufu makubwa kwenye eneo la kiungo?” alihoji.

Alipotafutwa Omog kuzungumzia lawama hizo, hakutaka kusema lolote, lakini msaidizi wake, Jackson Mayanja, alifafanua kwanini waliamua kumweka kando Jjuuko na kumchezesha Kotei katika nafasi ya beki wa kati.

“Tulikuwa tunamtegemea kwa sababu hatukuwa na namna ya kufanya kuweka mtu yeyote, lakini kama mchezaji akaliambia benchi la ufundi hayupo tayari kucheza kwa sababu amekaa muda mrefu bila kufanya mazoezi. Sisi tukawa hatuna namna, hatuwezi kumlazimisha mchezaji wakati ameshasema hayupo tayari tukakubaliana naye akakaa benchi,” alisema Mayanja.

Mayanja anasema tatizo halikuwa kwenye safu ya ulinzi, bali kwa washambuliaji ambao walipoteza nafasi nyingi za kufunga na kushindwa kuumaliza mchezo mapema.

“Najua nje ya uwanja kila mtu anasema jambo lake, lakini ukweli tunaujua sisi watu wa benchi la ufundi, tunapokea ushauri lakini wakati mwingine mtu anayekushauri hajui matatizo ya wachezaji, tulijua kabisa hatukuwa na Bukungu, hivyo Jjuuko alipaswa kuwa uwanjani, lakini haikuwezekana, Kotei pia si mbaya sana maana kwenye mechi ya Yanga alicheza nafasi hiyo baada ya kadi nyekundu na alifanya vyema,” anasema Mayanja.

Akizungumzia mbio za Ubingwa msimu huu, Mayanja alisema bado ubingwa ni mgumu sana na hautabiriki ingawa wao wanaongoza ligi na wanajipanga kumaliza ligi wakiwa kileleni.

“Ubingwa wa ligi kuu bado ni mgumu, hatujui nini kitatokea kwa Yanga, lakini hatujui pia matokeo yetu kwa mechi zijazo, tuna mechi kadhaa za ugenini ambazo ni ngumu,” alisema.

Source: Bingwa
Mashabiki Simba wamgeukia Joseph Omog Mashabiki Simba wamgeukia Joseph Omog Reviewed by Zero Degree on 3/06/2017 11:34:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.