Loading...

Simba yavunja rekodi

MCHEZO wa Kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali ulizozikutanisha timu ya Madini na Simba katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, umevunja rekodi baada ya kukusanya Sh 81,427,000.

Mashabiki walifurika kutazama mpambano huo, ambapo wengi wao pia hawakuweza kushuhudia kutokana na uwanja kukosa nafasi ya kuhimili idadi kubwa ya watu.

Katika mchezo huo, jumla ya watazamaji 14,056 walikata tiketi na kufanikiwa kuingia uwanjani wakati uwanja huo unabeba idadi ya watu 12,000, huku mashabiki wengine wakizuiliwa kutokana na usalama.

Kutokana na mapato hayo, Serikali ilifaidika kupitia kodi ya VAT baada ya kupata Sh 12,421,067, huku wamiliki wa uwanja ambao ni Chama cha Mapinduzi (CCM) walipata Sh 9,678,289, timu ya Madini ilipata Sh 16,130,483 na Simba kiasi kama hicho.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipata Sh12,904,386, Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA), Sh milioni 3.2 wakati gharama za mchezo ni Sh 6,452,193,na kufanya jumla ya mapato kuwa Sh 81,427,000 kutokana na watazamaji 14,056 waliolipa.

Mapato hayo haijawahi kutokea kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid tangu mwaka 1976 wakati Pan African ilipovaana na timu ya Vita kutoka Zaire.

Katibu wa siasa na uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe alisema kuwa kuna uharibifu wa mageti yalijitokeza kwenye mchezo huo na tayari watatumia mapato hayo kufanya ukarabati.

Aliongeza kuwa suala la kuufunga uwanja lilikuwa tangu mwezi uliopita japo ARFA iliomba zoezi hili lisitishwe ili ligi daraja la tatu ngazi ya Mkoa imalizike ndipo mambo menine yaendelee.

Mchezo huo wa Kombe la Shirikisho ulizikutanisha timu za Madini ya jijini hapa iliyochuana vikali na vinara wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara Simba ulimalizika kwa wenyeji kufungwa bao 1-0.
Simba yavunja rekodi Simba yavunja rekodi Reviewed by Zero Degree on 3/21/2017 03:55:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.