Loading...

Waziri aigiza NEMC kukifunga kiwanda cha saruji Moshi

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kukifunga kiwanda cha saruji cha Moshi mkoani Kilimanjaro, hadi maelekezo yaliyotolewa na baraza hilo yatakapotekelezwa.

January yuko ziarani katika mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania kukagua shughuli za mazingira.

Alitembelea kiwanda hicho akitokea ziarani Tanga, kutokana na malalamiko ya wananchi juu ya uchafuzi wa hewa itokanayo na vumbi katika shughuli za uzalishaji.

Akitoa maelezo wa awali, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agness Hokororo, alisema kiwanda hicho kimeendesha shughuli za uzalishaji wa saruji kwa kutofuata Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na mfumo mzuri wa kudhibiti uchafuzi unaotokana na vumbi kiwandani hapo.

Kwa upande mwingine, Dk Menan Jangu ambaye ni Mratibu wa Mazingira kutoka Nemc Kanda ya Kaskazini, alisema ofisi yake awali ilitembelea kiwanda hicho na kutoa mwongozo na taratibu zinazotakiwa kufuatwa kwa mujibu wa sheria hiyo ya mazingira.

“Tuliwaelekeza kujenga uzio kuzunguka kiwanda, kujenga njia maalumu za kupita na kuweka mashine maalumu ya kuzuia vumbi lisisambae kwa wingi angani, vitu ambavyo havijafanyiwa kazi,” alibainisha Dk Jangu.

Mwakilishi wa kiwanda hicho ambaye ni raia wa China, aliyefahamika kwa jina moja tu Sophia, alisema suala la kuzungusha uzio eneo lote litatekelezwa pindi hatimiliki ya ardhi ya eneo hilo itakapopatikana.

Hata hivyo, January aliagiza Nemc kukifunga kiwanda hicho mpaka mapendekezo yaliyotolewa na baraza hilo yatakapokamilika.

Katika hatua nyingine, alitembelea Ziwa Chala na kuwataka wadau wa mazingira kuongeza jitihada katika kulihifadhi kwa kuwa ni muhimu kwa ikolojia na historia yake.

“Kina cha ziwa hili kinashuka kwa kasi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na sisi kama Serikali tutahakikisha tunawekeza nguvu zetu katika kunusuru kina cha ziwa hili kisiendelee kushuka,” alisisitiza January.

Aliahidi kuzungumza na Serikali ya Kenya ili kuwa na mikakati ya pamoja ya kuhifadhi ziwa hilo kwa kuwa lipo katika pande za nchi hizo mbili.

Ziwa Chala ni chanzo kikubwa cha utalii na limetokana na mlipuko wa volkano likiwa halitoi wala kuingiza maji kutoka vyanzo mbalimbali.
Waziri aigiza NEMC kukifunga kiwanda cha saruji Moshi Waziri aigiza NEMC kukifunga kiwanda cha saruji Moshi Reviewed by Zero Degree on 3/28/2017 02:51:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.