Loading...

China yaajiri Watanzania 150,000

BALOZI wa China, Lu Youqing, amesema mpaka kufikia mwaka jana nchi yake ilikuwa imetoa ajira 150,000 kwa Watanzania baada ya kufanya uwekezaji wa dola za kimarekani bilioni 6.62 (sawa nash. trilioni 14.6).

Balozi Youqing aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa halfa ya utoaji wa zawadi kwa wafanyakazi wa kampuni za kichina na wanafunzi bora waliohudhuria programu ya mafunzo ya Tarajali kwenye kampuni za Kichina.

Alisema nchi yake imefanya uwekezaji huo kwamba zaidi ya Watanzania 350,000 pia wanafanya biashara kati ya China na Tanzania ikiwa ni sehemu ya kukuza uchumi na kuongeza maendeleo ya nchi.

“Kampuni nyingi za Kichina zimewekeza nchini Tanzania na zimeleta fedha, teknolojia na uzoefu wa utawala ambao unahitajika sana hapa Tanzania na pia zimefanikiwa kuzidisha maendeleo ya kiuchumi na uboreshaji wa kijamii nchini Tanzania,” alisema balozi huyo.

Balozi Youqing alisema Tanzania imeweka uzito katika suala la uboreshaji wa miundombinu na ujenzi wa viwanda kama mkazo wa kutimiza lengo la kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Alisema kuwa jambo hilo linahitaji kuongezeka kwa kasi ya kufundisha wafanyakazi wenye ujuzi bora ili kufikia malengo ya uchumi wa kati.

“(Hivyo) tulizitaka kampuni za kichina nchini Tanzania kuandaa shindano la ujuzi wa wafanyakazi Watanzania na programu ya mafunzo ya Tarajali kwa wanafunzi Watanzania,” alisema.

Aidha alisema nchi yake ina mkakati wa kuisaidia Tanzania kujenga kituo cha mafunzo ya kiufundi ili kutoa programu za mafunzo ya kina kwa wafanyakazi Watanzania na kufundisha wanafunzi wengi wenye ujuzi bora kwa maendeleo ya viwanda vya Tanzania.

Alisema wanafunzi waliopatiwa zawadi pamoja na wafanyakazi wamekuwa ni mfano bora kwa wachina na Watanzania kwenye kusaidiana na kubadilishana uzoefu.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi Tanzania kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. John Jingu alishukuru kuanzishwa kwa shindano hilo kwani limesaidia kuwajenga wanafunzi hao kiuwezo na kiuchumi. “Mafunzo waliyoyapata yataongeza ufanisi kwani vijana wetu wamejifunza umuhimu wa kufanyakazi kwa bidii kama inavyosisitizwa na Rais John Magufuli,” alisema Dk. Jingu.
China yaajiri Watanzania 150,000 China yaajiri Watanzania 150,000 Reviewed by Zero Degree on 4/23/2017 11:06:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.