Loading...

Lwandamina apewa kibarua kizito na Uongozi wa Yanga

UONGOZI wa Yanga umeibuka na kusema wakati huu Ligi ikiwa inaelekea ukingoni, hiyo ikiashiria kuwa pilikapilika za usajili zinakwenda kuanza, hawatamwingilia kocha wao, George Lwandamina, katika maamuzi yake.

Hayo yamezungumzwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, ambaye alisema siku zote kocha anapoingiliwa katika majukumu yake inaweza kuwa chanzo cha kufanya vibaya.

Mkwasa, ambaye ni kocha mzoefu, alisema hayo wakati huu ambapo baadhi ya wachezaji wake mikataba yao inaelekea ukingoni, akiwamo straika Mzimbabwe Donald Ngoma na Vincent Bossou, ambao taarifa zaidi zinadai kuwa wanaweza wakatimka zao.

Mbali na Ngoma na Bossou, pia kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, inasemekana kuwa ataondoka baada ya kupata timu nje ya nchi, huku taarifa nyingine zikidai kuwa wapo baadhi ya wachezaji watatemwa, akiwamo Ally Mustapha ‘Barthez,’ Haji Mwinyi Mngwali, Oscar Joshua na Justice Zullu.

Kwa upande wa wachezaji ambao huenda wakasajiliwa na mabingwa hao watetezi, inasemekana wamo kiungo wa Mbeya City, Kenny Ally na mwenzake, Mrisho Ngassa, Salim Hoza (Mbao FC), Misheck Chaila (Zesco FC, Zambia), Rashid Mandawa (Mtibwa) na Gadiel Michael (Azam FC).

Akiyazungumzia hayo, Mkwasa alisema: “Unajua linapokuja suala la usajili yanazungumzwa mambo mengi sana, lakini nikuambie tu, sisi hatutamwingilia kocha katika suala hilo, yeye tunampa jukumu la kuchagua nani abakie na nani aondoke,” alisema.

“Suala la nani atabaki au kuondoka hilo ni jukumu la kocha, suala la Ngoma na Bossou pia liko mikononi mwake, akihitaji huduma yao basi kamati husika itafanya majukumu yao ya kuzungumza nao,” alisema.
Lwandamina apewa kibarua kizito na Uongozi wa Yanga Lwandamina apewa kibarua kizito na Uongozi wa Yanga Reviewed by Zero Degree on 4/02/2017 03:56:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.