Loading...

Muhimu: Ni kuhusu Ugonjwa wa moyo, ...dalili na vyanzo vyake

TAKWIMU zilizopo zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wenye matatizo ya moyo wanaofanyiwa upasuaji katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ni watoto.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi anasema magonjwa mengi ya moyo kwa watoto ni yale yanayohitaji kufanyiwa upasuaji huku asilimia 65 ya watu wazima wanaotibiwa katika taasisi hiyo, wakitibiwa bila kufanyiwa upasuaji.

“Hii inatokana na kwamba, matatizo yao ni yale yanayohitaji kufanyiwa upasuaji ikiwa ni pamoja na tatizo la valvu za moyo,” anasema Profesa Janabi. Mwaka jana, Profesa Janabi anasema, taasisi hiyo ilihudumia wagonjwa 50,000 wa nje na ilifanya upasuaji kwa watu 1,000 wenye matatizo mbalimbali ya moyo.

Mtoto akifanyiwa upasuaji wa moyo na jopo la madaktari katika moja ya kambi maalumu za upasuaji unaofanywa na madaktari bingwa kwa njia ya vitundu vidogo katika Taasisi ya JKCI.
Aidha, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka taasisi hiyo, Dk Tulizo Shem anataja sababu zinazochangia matatizo ya moyo kwa watoto kuwa ni pamoja na kutopata matibabu vizuri na wakati mwingine, kunachangiwa na wadudu wanaosababisha mafua na matezi ya kooni.

Anasema ugonjwa wa matezi usipotibiwa vizuri husababisha athari kubwa katika valvu za moyo kwa watoto. “Watoto wa miaka 5 hadi 15, valvu zao zinaweza kupata shida ya kushindwa kufunga vizuri na kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi vizuri na ndio maana haya magonjwa yanafanyiwa upasuaji,” anasema Dk Shem.

Upasuaji unaofanywa katika tatizo hilo ni kuzisaidia valvu zitanuke ili ziweze kupitisha vizuri hewa na hivyo kumfanya mgonjwa kuweza kupumua vizuri kama alivyo mtu wa kawaida, upasuaji wa aina hii unafanywa katika taasisi hiyo kwa sasa kupitia vitundu vidogo bila kuwa na haja ya kufungua kifua.

Anasema watoto wanaotoka kwenye mikoa ya wafugaji ndio wanaoathirika zaidi kutokana na kutotibiwa kikamilifu magonjwa ya mfumo wa hewa ambayo huyapata kutokana na kulazwa na wanyama hivyo kutokuwa na mzunguko mzuri wa hewa safi.

“Mfano Mkoa wa Arusha tatizo ni kubwa zaidi katika mikoa hiyo, mtoto analazwa chumba kimoja na mifugo, vumbi linamfanya kupata matezi na mafua. Badala ya kuyatibu wanawapeleka kwa wazee wa kimila wanakwangua matezi wakiamini tatizo limekwisha,” anasema Shem.

Shem alizitaja sababu nyingine za mtoto kupata matatizo ya moyo katika umri mdogo kuwa ni pamoja na wengine kuwa na magonjwa ya kurithi yanayotokana na mama kutochunguza afya yake ili kuyatibu vizuri hasa anapokuwa mjamzito.

Sababu nyingine ni mama kupungukiwa madini ya folic acid pamoja na unywaji pombe wa kupitiliza hasa pombe kali, uvutaji sigara, matumizi ya dawa za kulevya na matumizi ya dawa bila ushauri wa daktari.

Dk Shem anasema ni vizuri mama kuchunguza afya yake mapema ikiwa ni pamoja na magonjwa mbalimbali ya maambukizo wakati wa ujauzito na kuhakikisha anatibiwa ili kuhakikisha hayamletei shida mtoto aliye tumboni. Anasema, mama anapaswa kufuata matumizi sahihi ya dawa wakati wa ujauzito na kutotumia dawa bila ushauri wa daktari kwani dawa zinaweza kumletea matatizo mtoto aliye tumboni.

“Kuna umri fulani ambao valvu zinatengenezwa hasa miezi mitatu ya mwanzo katika mimba, ni kipindi ambacho mama anatakiwa achunge sana afya yake, asijiingize kwenye kunywa dawa ovyo, ulevi, na ahakikishe anatibiwa magonjwa yote,” anasema Dk Shem.

Alisema kipindi hicho ni muhimu kwani viungo vya mtoto vinakuwa vinatengenezwa, hivyo kuharibika baadhi ya viungo na ni vigumu kuvitengeneza ikiwa ni pamoja na valvu za moyo wa mtoto. Aidha, Shemu aliwaasa pia wanawake kupata watoto katika umri sahihi kuepuka kuzaa wakiwa na umri mkubwa unaosababisha magonjwa kwa mtoto ikiwa ni pamoja na tatizo la moyo.

Anasema hali ya baadhi ya watoto kuzaliwa na matatizo ya mapungufu kimaumbile au dosari katika baadhi ya viungo vya ndani au nje katika mwili wa mtoto, hutokana na kuzaliwa na mama mwenye umri mkubwa.

Asilimia kubwa ya watoto wanaotibiwa katika taasisi ya JKCI mbali na kurithi na kutopata matibabu sahihi ya magonjwa kwa watoto, pia yapo yanayotokana na mfumo wa maisha yaani ulaji usiofaa na pia kutofanya mazoezi. Anasema watu wazima wengine wanabainika kuwa na tatizo la moyo wakiwa watu wazima, lakini tatizo hilo likiwa ni la kurithi yanajitokeza katika umri wa utu uzima.

Daktari Bingwa katika taasisi hiyo, Dk Pe’dro Pallangyo anasema tatizo la valvu za moyo ni asilimia 15 ya wagonjwa wote wanaofika kutibiwa hapo. “Hii inatokea mtu kupata maambukizi ya mafua na wale wadudu kuzaliana kwa wingi baadaye kuingia kwenye mfumo wa damu kisha kwenda kushambulia valvu za moyo na kushindwa kufanya kazi,” alisema.

Pallangyo anasema tatizo hili linawapata watu ambao ni wa umri mdogo kabisa. Aliwaasa wazazi kuzingatia afya za watoto wao bila kupuuza ugonjwa unaojitokeza kwa mtoto. Anasema watoto wenye umri kati ya siku moja hadi miaka mitano wanakabiliwa na kubwa ya matatizo ya tundu kwenye moyo, mishipa ya damu kuchomoza kwenye moyo sehemu ambayo haistahili na tatizo la valvu.

Pallangyo anasema mama anapokuwa mjamzito anatakiwa kuepuka vihatarishi vyote, ikiwa ni pamoja na uvutaji sigara, kukaa karibu na mtu anayevuta sigara, unywaji wa pombe. Anasema mama azingatie kupima afya yake na kupata madini chuma. Ugonjwa mwingine wa moyo hujulikana kwa jina Rheumatic Heart Disease.

Huu ni ugonjwa unaoharibu valvu za moyo ambazo zipo 4. Congenital Heart Diseases, haya ni magonjwa ya moyo ambayo mtoto anazaliwa nayo, na mara nyingi huzaa vifo kwa watoto. Inakadiriwa kwamba watu karibu milioni 17.5 hufariki dunia kila mwaka kwa magonjwa ya moyo, yakifuatia magonjwa ya saratani milioni 8.2 kwa mwaka, wakati magonjwa ya njia ya hewa milioni nne na kisukari watu milioni 1.5 kila mwaka.

Takwimu za Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania (PAT) zinaonesha kwamba, watoto 13, 600 huzaliwa kila mwaka wakiwa na magonjwa aina mbalimbali ya moyo. Wastani wa watoto 3,400 kati ya hao, huhitaji kupatiwa matibabu kwa kufanyiwa upasuaji.

Dalili kuu za magonjwa ya moyo zinazojitokeza ni pamoja na maumivu ya kifua upande wa kushoto, moyo kwenda mbio, kukosa pumzi au kushindwa kupumua, kuvimba miguu, tumbo na mishipa ya shingoni kujitokeza nje. Dalili nyingine ni maumivu ya mgongo, mabega, shingo na taya, kichefuchefu na kutapika, kukosa usingizi, kupoteza fahamu na kikohozi kisichokwisha.

Hata hivyo, kutokeza kwa mambo hayo ni dalili kwamba mtu huyo amekuwa akiishi na ugonjwa kwa muda mrefu. Wataalamu wa magonjwa ya moyo wanashauri kuwa, mtu anapohisi maumivu ya aina yoyote kifuani, hasa baada ya kufanya mazoezi, ni muhimu kuonana na daktari haraka.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2011, vifo vilivyotokana na magonjwa ya moyo nchini Tanzania ni 19,083. Takwimu hizi zinaiweka Tanzania katika nafasi ya 87 duniani kati ya nchi karibu 200.

Kutokana na ukubwa wa tatizo la magonjwa ya moyo, mwaka 2008 Serikali iliamua kuanzisha huduma ya upasuaji mkubwa wa moyo na hatimaye kujenga Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), ambayo iliyoanza kazi mwaka 2015.
Muhimu: Ni kuhusu Ugonjwa wa moyo, ...dalili na vyanzo vyake Muhimu: Ni kuhusu Ugonjwa wa moyo, ...dalili na vyanzo vyake Reviewed by Zero Degree on 4/06/2017 11:52:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.