Loading...

Serikali yalaani kitendo cha kushambuliwa kwa wanahabari katika mvutano wa CUF

Mkurugenzi wa Habari Maelezo, Hassan Abbas
Serikali imesema imepokea kwa masikitiko taarifa za kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya waandishi wa habari katika mvutano uliotokea Jumamosi, jijini Dar es Salaam kati ya wafuasi wa pande mbili zinazokinzana za Chama cha Wananchi (CUF).

Serikali, kupitia Mkurugenzi wa Habari Maelezo, Hassan Abbas imetoa taarifa leo ikisema serikali itachukua muda kidogo kulifuatilia suala hili na kubaini chanzo. Licha ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti polisi, wapo waandishi ambao vifaa vyao vya kazi pia vililengwa katika mashambulizi hayo.

“Tunachukua fursa hii, kulaani kitendo cha kuumizwa wanahabari waliokuwa wamealikwa kuhudhuria mkutano huo wa CUF. Ifahamike kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii,” imeeleza taarifa hiyo.

“Kifungu cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwepo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa. Misingi ya uhuru huu wa kitaaluma pia imesisitizwa katika Ibara za 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu imeuridhia.”

“Tunawatakia nafuu ya haraka wanahabari waliojeruhiwa na wenzao wengine waliopatwa na jakamoyo katika tukio hilo. Kwa kuwa suala hili tayari limeripotiwa polisi, tunawaomba wadau wote wa habari na wanasiasa kwa sasa kutulia na kuviachia vyombo husika vilifanyie kazi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe,” imefanua taarifa hiyo.
Serikali yalaani kitendo cha kushambuliwa kwa wanahabari katika mvutano wa CUF Serikali yalaani kitendo cha kushambuliwa kwa wanahabari katika mvutano wa CUF Reviewed by Zero Degree on 4/24/2017 02:40:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.