Loading...

Usajili ulivyoibua zengwe ndani ya Klabu ya Yanga

WAKATI zoezi la usajili wa wachezaji likitarajiwa kuanza kwa ajili ya msimu mpya wa majira ya kiangazi, tayari zengwe limeibuka ndani ya Klabu Bingwa ya Soka Tanzania, Yanga.

Zengwe hilo linatokana na msimamo mkali uliowekwa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa, ambaye amesisitiza watafanya usajili mzito utakaokuwa na malengo ya kuisaidia timu, huku akiwatahadharisha ‘wapiga dili’ kutokuwa na nafasi kwenye usajili msimu huu.

Mkwasa aliyasema hayo jana, alipokuwa anazungumza na gazeti hili na kusisitiza kuwa atahakikisha anaipa heshima kubwa klabu hiyo kwa kufanya usajili utakaokuwa na tija na si ili mradi tu usajili.

Alisema kuwa, kikubwa atakachokifanya ni kwenda kisayansi zaidi, ikiwamo kuandika ripoti zitakazokuwa na malengo mazuri katika suala zima la usajili na kamwe hataruhusu usajili wa asilimia kumi katika kikosi cha msimu ujao.

“Nipo Yanga kuipa heshima, niliwahi kuwa mchezaji, kocha na sasa Katibu, naelewa masuala mengi jinsi yalivyoendeshwa huko nyuma, imefika wakati sasa na mimi niisaidie Yanga na kuipa heshima yake,” alisema Mkwasa.

Alisema katika utendaji wake hakutakuwa na usajili usiokuwa na malengo, ambao unalenga kuwanufaisha watu wachache na kusisitiza usajili wa msimu ujao utazingatia zaidi matakwa ya benchi la ufundi.

Akizungumzia suala la 10%, Mkwasa alisema kama limekuwa likifanyika basi si katika msimu huu chini ya utawala wake, kwani suala hilo ndilo limekuwa likizifanya timu za Tanzania kuleta wachezaji wa kigeni wasiofaa ambao wanazidiwa kiwango na wachezaji wa ndani.

Kuhusu kuundiwa zengwe na baadhi ya watu, Mkwasa alisema hajui hilo, anachokijua ni kufanya kazi kwa mujibu wa makujumu yake na kwa lengo la kuisaidia Yanga kupiga hatua.

Katika hatua nyingine, alipoulizwa kuhusu zengwe linaloundwa na baadhi ya wajumbe wa kamati ya mashindano, Mkwasa alisema kubwa linalomuweka Yanga ni kuhakikisha anafanya kazi kwa weledi.

“Kama suala hilo lipo haina tatizo, kila mtu ana utashi wake wa kuongea na kupinga, lakini nikwambie kitu, nitajitahidi kuifanya Yanga kuwa ya kisayansi zaidi kwa kuzingatia weledi,” alisema.

Lakini BINGWA ilikwenda mbali zaidi na kumtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Yanga, Mhandisi Paul Malume, ili kujua kiundani suala hilo, alisema kuwa, suala la kuondolewa Mkwasa kwake bado hawajalisikia.

“Hili suala mimi bado sijalisikia, kwanza nilikuwa kijijini likizo, nimeanza kazi Jumatatu hii na sijakwenda klabuni, kwahiyo sijui lolote mpaka nifike klabuni,” alisema Malume.

Kwa upande wake, mwanachama maarufu wa timu hiyo, Sudi Tall, alipoulizwa kuhusu tetesi hizo za kuundiwa zengwe Mkwasa alisema: “Kama kuna jambo ambalo Wanayanga watalijutia ni kuanza kumpiga mizengwe Mkwasa, kwani ni mtu makini ambaye anaujua uchungu wa timu hiyo.

“Mkwasa ameipigania Yanga hadi kufikia hatua ya kuchanika uso, kuumia magoti akiwa mchezaji kabla ya Mohamed Viran ‘Babu’ kumpeleka Ulaya kwenda kusomea ukocha na leo wanafaidi matunda yake, tuache chokochoko jamani,” alisema.

Mkwasa kwa siku za karibuni amejikuta akiwa kiongozi mwenye weledi ndani ya klabu hiyo, baada ya kuamua kuanzisha mfumo mpya wa uchangiaji wa timu hiyo ili kujikwamua kiuchumi, mfumo unaokwenda vema mpaka sasa.


Source: Bingwa
Usajili ulivyoibua zengwe ndani ya Klabu ya Yanga Usajili ulivyoibua zengwe ndani ya Klabu ya Yanga Reviewed by Zero Degree on 4/28/2017 03:24:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.