Loading...

Wananchi waililia Serikali wakitaka mgao kutoka katika pato la utalii

WANANCHI wanaoishi Tarafa ya Ngorongoro wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, hawajakata tamaa na kuendeleza kilio chao kwa serikali kwa kuomba kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kuweka utaratibu mbadala wa kuwalipa kiasi cha fedha kinachotokana na utalii ili kuwanusuru na njaa kali inayowakabili.

Taarafa hiyo yenye zaidi ya wakazi 82,000 kati ya hao asilimia tatu tu ndio wenye uwezo wa kufuga, huku asilimia 97 wakiwa hawana uwezo wa kufanya chochote kutokana na wananchi hao kuzuiwa kufanya shughuli zozote za kilimo ndani ya hifadhi hiyo.

Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nainokanoka, Edward Maura akizungumza katika kikao cha kuwanusuru wananchi hao na baa la njaa, alisema wananchi wa tarafa hiyo wapo katika hali ngumu kimaisha kutokana na kutokuwa na njia yoyote mbadala ya kuwaingizia kipato huku wakitegemea chakula la msaada kutoka NCAA ambacho hakiwatoshelezi.

“Pamoja na kuahidiwa kuletewa chakula wakati mwingine hakifiki kabisa na hakitoshi tunaiomba sana serikali kwa kushirikiana na NCAA waweke utaratibu wa kutulipa fedha zinazotokana na utalii kila mwezi angalau Sh 300,000 kwa kila kaya ili waweze kujikimu kimaisha vinginevyo maisha yanazidi kuwa hatarini,” alieleza. Naye Meneja Mipango wa Baraza la Wafugaji Wanawake (PWC), Alais Melau alisema wamekuwa wakiwajengea uwezo vikundi vya akina mama na kuwapatia mikopo na kuanzisha miradi midogo midogo ya kujikwamua kiuchumi.

Melau alisema wamewagawia wananchi hao mbuzi 900 na kuwasaidia kuanzisha maboma ya kiutamaduni ambayo wamekuwa wakifanya shughuli za utalii na kujipatia kipato cha kuendeleza familia zao. Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Ngorongoro, William ole Nasha alisema matatizo yanayowakabili wananchi wa taarifa hiyo ni kutokana na kuwepo kwa sheria ya ardhi inayowanyima uhuru ndani ya hifadhi hiyo

. Alisema katika kuhakikisha kuwa wananchi hao wanaondokana na njaa, wameandaa utaratibu kuwaletea wananchi chakula na kuwauzia kwa bei nafuu ya soko ili kila mwananchi amudu gharama za kununua chakula hicho.


Source: Habari Leo
Wananchi waililia Serikali wakitaka mgao kutoka katika pato la utalii Wananchi waililia Serikali wakitaka mgao kutoka katika pato la utalii Reviewed by Zero Degree on 4/18/2017 07:27:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.