Loading...

Kodi 108 sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, katika mwaka wa fedha 2017/18 zimefutwa

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba
WIZARA ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, katika mwaka wa fedha 2017/18, imeshusha neema kwa watanzania kwa kufuta kodi 108 zilizokuwa kero kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini. Kati ya tozo hizo zilizofutwa, 80 ni tozo za tasnia ya kilimo pekee kati ya 139, uvuvi wamefutiwa tozo tano na mifugo wamefutiwa tozo 23.

Pamoja na hayo wizara hiyo katika kutengeneza ajira na kuongeza mapato ya nchi, imefanyia marekebisho baadhi ya kanuni za Mamlaka ya kusimamia Uvuvi wa bahari kuu, na moja ya kanuni hizo ni kuanzia sasa kila meli ya kimataifa ya uvuvi italazimika kuajiri vijana wa kitanzania kufanyakazi kwenye meli hizo.

Hayo yalisemwa bungeni Dodoma jana na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk Charles Tizeba, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2017/18. Dk Tizeba alisema katika maamuzi hayo kwenye tasnia ya tumbaku jumla ya tozo 10 zilifutwa na tozo mbili kupunguzwa viwango.

Baadhi ya tozo hizo zilizofutwa ni mchango wa Ushirika wa Mkoa wa thamani ya Dola za Marekani 0.072 (Sh 151.2) kwa kilo. Nyingine ni mchango kwa chama cha ushirika kwa kiwango cha dola za Marekani 0.030 (Sh 63) kwa kilo, mchango kwa ajili ya gharama za masoko ya ushirika kiwango cha dola 0.070 (Sh 147) kwa kilo, dhamana ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mikopo kwa kiwango cha asilimia moja na fomu ya maombi ya leseni za Tumbaku kwa kiwango cha dola 100 (Sh 210,000).

Kodi nyingine za tumbaku zilizofutwa ni kodi ya leseni kununua tumbaku kavu kwa kiwango dola 4,000 (Sh milioni 8.4), leseni ya kununua Tumbaku mbichi kiwandani kwa kiwango cha dola 4,000, leseni ya kununua Tumbaku mbichi kwa kila wilaya kiwango cha dola 3,500 (Sh milioni 7.3), leseni ya kuuza Tumbaku nje ya nchi kiasi cha dola 4,000 na tozo ya Baraza la Tumbaku kiasi cha dola 0.01 kwa kilo.

Pia kupitia zao hilo za tumbaku, kodi zilizopunguzwa ni pamoja na kodi ya leseni ya kununua tumbaku kavu ambayo ni dola 4,000 imepunguzwa kwa asilimia 50 na kuwa dola 2,000 (Sh milioni 4.2) na leseni ya kusindika tumbaku kiasi cha dola 10,000 (Sh milioni 21) iliyopunguzwa kwa asilimia 50 na kuwa dola 5000 (Sh milioni 10.5). Aidha, alisema katika tasnia ya kahawa, jumla ya tozo 17 zitafutwa na tozo moja itapunguzwa kiwango.

Baadhi ya zilizofutwa ni ada ya leseni ya kuuza nje ya nchi kahawa ya kijani kwa kampuni na vyama vya ushirika kiwango cha dola 1,000 (Sh milioni 2.1). Nyingine ni makato ya asilimia 0.75 ya bei ya kahawa mnadani kwa ajili ya kugharamia shughuli za utafiti wa kahawa, ada ya leseni ya ghala la kahawa kwa kampuni na vyama vya ushirika kiwango cha dola 500 (Sh milioni 1.05), ada ya leseni ya Premium Coffee kwa kampuni kiwango cha dola 1000 na kupunguza kwa asilimia 50 makato ya asilimia 0.75 ya bei ya kahawa mnadani.

Akizungumzia tasnia ya sukari alisema jumla ya tozo 16 zitafutwa na baadhi yake ni ada ya leseni uingizaji wa sukari ya viwandani kwa kiwango cha Sh 200,000, ada ya leseni ya uingizaji wa sukari ya kuziba pengo kwa kiwango cha Sh 200,000 na ada ya leseni kamili ya uzalishaji sukari uwekezaji mkubwa mpya kiwango cha dola 30,000 (SH milioni 63).

Alisema katika tasnia ya pamba tozo zitakazofutwa ni mbili ambazo ni tozo ya Kituo cha kununulia pamba katika ngazi ya Halmashauri (Sh 5,000) na tozo ya maendeleo ya elimu inayotozwa kwa kiwango cha Sh 10 kwa kilo katika Halmashauri ya Meatu.

Katika tasnia ya korosho tozo mbili ambazo ni gharama za magunia na kamba Sh 56 kwa Kilo na ada ya leseni ya kununua Korosho kiwango cha dola za Marekani 1,000 zilifutwa huku tozo moja ya chai ikifutwa ambayo ni gharama za uendeshaji wa Vyama vya Wakulima Sh tano kwa kilo.

Tozo tatu za mbolea zilizofutwa ni tozo kwa ajili ya usajili wa mfanyabiashara wa mbolea kiasi cha dola 50, ada ya leseni ya mfanyabiashara kiasi cha dola 20 na ada ya usajili wa mzalishaji cha dola 1,000 na moja iliyopunguzwa kiwango ni dola 1,000 za uhakiki wa ubora wa mbolea badala ya dola 30,000 za awali. Dk Tizeba alieleza kuwa katika kuimarisha maendeleo ya Ushirika nchini, Serikali itafuta tozo 20 zilizokuwepo katika Ushirika katika ngazi mbalimbali.

Baadhi ya tozo hizo ambazo hadi Julai Mosi, mwaka huu zitakuwa hazitozwi ni ada ya usajili wa marekebisho ya mashari ya chama cha ushirika cha msingi ya kiwango cha Sh 20,000, ada ya usajili wa marekebisho ya chama cha ushirika cha upili ya kiwango cha Sh 40,000 na ada ya usajili wa marekebisho ya chama cha ushirika cha kati ya Sh 80,000.

Kwa upande wa sekta ya mifugo, waziri huyo alitaja kodi zilizofutwa kuwa 23 zinazogusa tasnia za maziwa mbili, nyama 14 ma huduma za afya ya mifugo 17. Baadhi ya kodi hizo zilizofutwa ni ada ya usajili wa wadau kwa wazalishaji na wakusanyaji maziwa, kwa upande wa nyama zilizofutwa ni ada ya usajili wa wafugaji wakubwa ambayo ni Sh 75,000, wakati Sh 50,000 na wadogo Sh 15,000, ada ya usajili wa minada ya awali Sh 30,000 na minada ya upili na mpakani 50,000.

Katika eneo la huduma za afya za mifugo, kodi zilizofutwa ni tozo ya kibali cha kuingiza ngozi za ngo’mbe kwa kipande cha Sh 5,000, tozo ya kuingiza ngozi ya mbuzi au kondoo Sh 200 na tozo ya kibali cha afya cha kusafirisha ngómbe ndani ya wilaya 1,000, kondoo Sh 500, farasi au punda 750 na nguruwe 1,000. Akizungumzia sekta ya uvuvi kodi zilizofutwa ni tano na moja imeongezwa viwango.

Baadhi ya tozo zilizofutwa ni ushuru wa kuuza kaa hai nje ya nchi ni dola 0.60 kwa kilo, tozo ya movement permit, ada ya ukaguzi wa kina wa kiwanda kila robo mwaka Sh 100,000 na ada ya usajili wa chombo cha uvuvi ya mita 11 kwa wavuvi.

Pamoja na tozo hizo zilizofutwa na kupunguzwa, pia waziri huyo alizungumzia hatua iliyochukuliwa ya kurekebisha kanuni za mamlaka ya kusimamia uvuvi ambapo kuanzia Julai Mosi, mwaka huu meli zinazokata leseni za uvuvi wa bahari kuu zitatakiwa kushusha samaki wasiolengwa katika bandari ya Tanzania.

Pia meli hizo zitatakiwa kutozwa mrabaha kwa samaki watakaovuliwa katika bahari kuum kuruhusu uvuvi wa kukokota kwa nyavu za juu na kuajiri vijana wa kitanzania kufanyakazi katika meli hizo.

Waziri huyo alisema, pia serikali katika jitihada zake za kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa mbolea nchini katika msimu wa mwaka 2017/18 itaanzisha mfumo mpya wa kuagiza mbolea kwa pamoja.

Katika bajeti hiyo, wizara hiyo imeomba kupitishiwa bajeti ya Sh bilioni 267 kwa ajili ya fedha za kawaida na maendeleo, kati ya hizo Sh bilioni 111 ni fedha za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 156 za maendeleo.
Kodi 108 sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, katika mwaka wa fedha 2017/18 zimefutwa Kodi 108 sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, katika mwaka wa fedha 2017/18 zimefutwa Reviewed by Zero Degree on 5/21/2017 03:01:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.