Loading...

Lundenga hatarini kuzuiliwa kuandaa mashindano ya Miss Tanzania

Mkurugenzi wa kampuni ya LINO AGENCY, Hashim Lundenga 
SERIKALI imetishia kuifuta Kampuni ya Lino Agency katika uandaaji wa shindano la Miss Tanzania ikiwa itashindwa kutoa zawadi kwa mshindi wa mwaka 2016/17, Diana Edward.

Akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake bungeni mjini hapa juzi, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura, aliitaka kampuni hiyo iliyo chini ya Mkurugenzi Hashim Lundenga kumkabidhi zawadi ya gari Diana mara moja kabla serikali haijachukua hatua zaidi.

Diana alitwaa taji hilo Oktoba 26, mwaka jana katika fainali ya shindano hilo lililofanyika jijini Mwanza.

Wambura alisema kampuni hiyo inapaswa kutoa zawadi kwa mrembo huyo kufikia Juni mwaka huu.

Naibu Waziri huyo alisema iwapo kampuni hiyo itashindwa kutii agizo hilo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuiondoa katika uandaaji wa shindano hilo.

Mbali na zawadi ya Diana, Naibu Waziri huyo alisema kampuni hiyo pia inapaswa kuwapa zawadi warembo wengine waliofanya vizuri katika shindano hilo mwaka huu, lakini bado hawajapewa stahiki zao.

“Serikali imepitia na kufanya marekebisho ya dosari mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza katika mashindano ya urembo na hasa shindano la Miss Tanzania na kutoa agizo kwa mwandaaji na kama atashindwa kufanya hivyo atapoteza sifa za kuandaa,” alisema Wambura. 

Nipashe inafahamu kwamba, warembo walioshika nafasi nne za juu nao bado wanadai na fedha zao zimekuwa zikilipwa kwa mafungu kutoka Sh. milioni 18 wanazostahili kulipwa na sasa zimebaki Sh. milioni sita.

Mbali na Diana, warembo wengine wanaoidai Kamati ya Miss Tanzania ni aliyeshika nafasi ya pili, Grace Malikita, mshindi wa tatu Maria Peter, mshindi wa nne na wa tano.

Wambura aliliambia Bunge kuwa serikali haitafumbia macho ukiukwaji wa utamaduni wa Mtanzania unaofanywa na baadhi ya wasanii wa filamu nchini ambao wakati wa mjadala walilalamikiwa na baadhi ya wabunge kwa kuvaa 'nusu uchi'.

Alisema serikali haijazuia wala haitazuia kazi za filamu za nje ila inataka kazi hizo ziangaliwe kama zinaendana na utamaduni wa Kitanzania.

“Serikali haitakubali kuona utamaduni wa Mtanzania unakiukwa na ndiyo maana tumekuwa tukisisitiza maadili kwa ajili ya kudumisha utamaduni wetu,” alisema. 
Lundenga hatarini kuzuiliwa kuandaa mashindano ya Miss Tanzania Lundenga hatarini kuzuiliwa kuandaa mashindano ya Miss Tanzania Reviewed by Zero Degree on 5/10/2017 09:58:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.