Loading...

Madhara ya kumrusha mwanao darasa

Picha ya mtandaoni
KUMRUSHA mtoto darasa kwa kisingizio kwamba ana uwezo mkubwa ni jambo la hatari na linaweza kuharibu akili yake kadri anavyoendelea kukua na kupanda darasa, imeelezwa.

Mratibu na Mkufunzi wa Taasisi ya kutetea haki za watoto ya Tukumbushane Society, Celvin Shola aliwashauri wazazi kuacha kuwapangia walimu darasa gani watoto wao wasome kuondoa uwezekano wa kuwavuruga watoto wao kiakili.

Alikua akizungumza kwenye semina kuhusu mitaala mipya ya elimu ya awali kwa walimu wa shule za msingi wilayani Temeke Mkoa wa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Alisema hata kama mtoto ana kipaji na uelewa wa haraka si jambo jema kumrusha darasa ambalo si lake kwa sababu kila umri una tabia yake.


“Tabia hii ya kuwarusha watoto darasa kwa kisingizio kwamba wana akili sana imeshamiri katika shule hizi za English Medium (shule zinazofundisha kwa lugha ya kiingereza), huko baadhi ya wazazi wanapanga watoto wao wasome nini, waingie darasa lipi.

“Kisaikolojia akili ya mtoto inatakiwa kusoma vitu vinavyoendana na umri wake, hata kama mtoto yuko darasa la kwanza na ana uwezo wa kufanya mtihani wa darasa la tatu na zaidi, tuwashauri wazazi wasione kurusha mtoto darasa ni jambo la sifa, mwisho wake si mzuri.” alisema Shola bila kufafanua. 

Kuhusu elimu ya awali, Shola ambaye pia ni mkufunzi wa taasisi hiyo, alisema kwa kuwa Tanzania haikuwa na sera maalum na iliyokuwa wazi kuhusu elimu ya awali, imejikuta hata walimu wa kufundisha elimu hiyo hawapo au ni wachache.

Alisema walimu wengi nchini hawajapitia taaluma ya namna ya kufundisha elimu ya awali matokeo yake watoto wengi wanakosa haki ya msingi ya kujengwa akili kuanzia ngazi hiyo.

“Katika maeneo mengi ya vijijini elimu ya awali inafundishwa na walimu wenye umri mkubwa ambao wamestaafu au wanakaribia kustaafu na hawaendani kabisa na sifa zinazotakiwa katika kufundisha watoto wenye umri mdogo.

“Watoto wa awali lazima watumie muda mwingi kucheza na kuimba, kuchora na vitu vingi vya kuwafanya wapende shule, sasa huyu mtu mzima atawezaje vitu hivi? Anaweza kuruka kamba au kukimbia na hawa watoto?“ alihoji Shola.

Credits: Mtanzania
Madhara ya kumrusha mwanao darasa Madhara ya kumrusha mwanao darasa Reviewed by Zero Degree on 5/23/2017 12:12:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.