Loading...

Majeruhi wa ajali ya basi la Lucky Vincent ya Arusha akaribia kutembea

MMOJA wa majeruhi watatu wa ajali ya basi la wanafunzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Lucky Vincent ya Arusha ambaye alipelekwa nchini Marekani akiwa hana hisia kwenye miguu, ameanza kupata nafuu.

Taarifa iliyotolewa na Lazaro Nyalandu jana ilisema Doreen Mshana alianza kupata hisia kwenye miguu yote miwili kuanzia jana hiyo.

Doreen juzi alifanyiwa upasuaji uliodumu kwa saa nne na madaktari wa Hospitali ya Mercy iliyo katika Jiji la Sioux jimboni Iowa nchini humo.

Nyalandu ambaye ni Mbunge wa Singida Kaskazini, na mmoja wa waasisi wa Taasisi ya Elimu na Afya (STEM) iliyoratibu safari ya majeruhi hao kwenda Marekani, alibainisha kuwa hiyo ni hatua nzuri kwa Doreen kuelekea kumudu tena kutembea.

Doreen, Saidia Ismail na Wilson Tarimo wapo nchini Marekani kwa ajili ya matibabu ambayo yamewezeshwa na STEM na Serikali ambayo pia imepokea misaada inayodhaniwa kufikia Sh. milioni 68 kutoka kwa wahisani mbalimbali.

Doreen alifanyiwa upasuaji mkubwa wa uti wa mgongo baada ya kupata ajali mbaya hiyo ya gari ambayo ilisababisha vifo vya wanafunzi wenzake 32, walimu wawili na dereva wa shule hiyo.

Ajali hiyo ilitokea Mei 6 eneo la Malera wilayani Karatu, majira ya saa tatu asubuhi wakati mvua ikinyesha, baada ya basi la shule kushindwa kufunga breki likiwa kwenye mteremko, kuserereka na kutumbukia kwenye korongo.

Mwalimu wa shule hiyo, Efraim Jackson alisema gari hilo halikuwa na hitilafu na kwamba anadhani ukungu uliokuwapo katika eneo la ajali na ugeni wa madereva na barabara hiyo ndiyo vyanzo vya mkasa huo.

Wanafunzi waliofariki dunia walikuwa kwenye gari aina ya Mitsubishi Rosa lenye namba za usajili T871 BYS, mali ya shule hiyo.

Wanafunzi waliofariki katika ajali hiyo na ambao waliagwa kwa heshima zote kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kabla ya kuzikwa mwakwao ni Mtenge Amos, Justine Alex na Irine Kishari.

Wengine ni Gladness Goodluck, Praise Roland na Shadrack Biketh.

Wengine ni Junior Mwashuya, Aisha Said, Oumliqh Heri Rashid, Gema Gerald, Rebecca Daudi, Hagai Lucas, Sada Ally, Ruth Ndemna, Musa Kassim, Neema Elimaki na Neema Marten.

Wengine ni Grayson Robson Massama, Witness Mosses, Hevenight Enock, Las Tarimo, Arnold Alex, Naomi Hosea, Rukia Altami, Eliapenda Eliudi, Marion Mrema, Rehema Msuya, Subrina Said na Prisca Charles.

Wanafunzi hao wa darasa la saba walikuwa wakienda kufanya mitihani ya pamoja ya kujipima na wanafunzi wenzao wa Shule ya Tumaini Junior ya Karatu.
Mwalimu Jackson, alisema waliondoka Arusha kwenda Karatu majira ya saa 11 alfajiri wakiwa na wanafunzi 96.

Walifanya hivyo ili wawahi kwenda kufanya mtihani wa ujirani mwema, wakiwa kwenye magari matatu na kwamba gari la mwisho ndilo lililopata ajali na kusababisha vifo hivyo.

Alisema kuwa wakati wanaondoka hakukuwa na gari lolote lenye hitilafu, lakini kutokana na ukungu uliokuwapo katika eneo hilo ndilo lililosababisha ajali na ugeni wa madereva na barabara hiyo.

Alisema njiani hali ya hewa ilikuwa mbaya huku mvua ikinyesha muda wote.
Majeruhi wa ajali ya basi la Lucky Vincent ya Arusha akaribia kutembea Majeruhi wa ajali ya basi la Lucky Vincent ya Arusha akaribia kutembea Reviewed by Zero Degree on 5/22/2017 12:29:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.