Majibu ya Bocco kuhusiana na habari zilizozagaa mitandaoni kuanzia Ijumaa iliyopita
Nahodha wa Azam FC, John Bocco, hivi karibuni amejikuta ikiingia matatizoni na uongozi wa klabu yake hiyo baada ya wajanja wa mtandaoni kumzidi ujanja.
Ukurasa wa Instagram wa Bocco, Ijumaa iliyopita ulivamiwa na matapeli wa mtandaoni na kuanza kuandika mambo mbalimbali kuhusiana na mchezaji huyo, jambo ambalo liliushitua uongozi wa klabu hiyo.
Moja kati ya mambo hayo yaliyoandikwa katika ukurasa huo ni: “Kuna wakati wa kuondoka hata kama hujui pa kwenda, ondoka wajue thamani yako.”
Maneno hayo yaliwachanganya vilivyo viongozi wa timu hiyo, baada ya kuyaona katika ukurasa huo, jambo ambalo lilisababisha wamuulize alikuwa akimaanisha nini.
Bocco amesema kuwa, hali hiyo ilimsababishia usumbufu mkubwa kwani watu wengi waliamini kuwa yeye ndiye aliyeandika maneno hayo licha ya kuwaambia ukweli kuhusiana na kilichotokea.
“Nawaomba watu wote waelewe kuwa sina tatizo na Azam na wala siyo mimi niliyeandika maneno hayo, bali ni matapeli ambao wamevamia ukurasa wangu Instagram tangu juzi (Ijumaa) na wamekuwa wakiandika mambo yao hayo huku nikiona.
“Hata hivyo nimeshatoa taarifa sehemu zinazohusuka lakini pia nimeamua kufungua ukurasa mwingine wa Instagram,” alisema Bocco ambaye anadaiwa mkataba wake na Azam umemalizika, hivyo inadaiwa kuwa ametumia mbinu hiyo ili kuushitua uongozi wake uweze kumpatia mkataba mwingine.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alisema: “Huo ni uzushi tu ambao hauna ukweli wowote, mimi bado nina mkataba na Azam na kama utamalizika na wakiwa bado wananihitaji wataniambia, hivyo siwezi kufanya hivyo hata siku moja.”
Viongozi wa Azam FC hawakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hilo, kutokana na simu zao za mkononi kuita tu bila ya kupokelewa.
Source: Champion
Majibu ya Bocco kuhusiana na habari zilizozagaa mitandaoni kuanzia Ijumaa iliyopita
Reviewed by Zero Degree
on
5/22/2017 11:41:00 AM
Rating: