Loading...

Polisi waua ‘Jambazi’ wakati akijaribu kupora fedha za Benki ya CRDB

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema jana Mei 14, 2017 majira ya asubuhi maeneo ya Kurasini katika jengo la Makao Makuu ya Uhamiaji lilifanikiwa kumjeruhi kwa risasi jambazi mmoja aliyekuwa akijaribu kumnyang’anya silaha askari aliyekuwa akisindikiza gari la kampuni ya G4S lililokuwa limebeba fedha Tsh. 320,000,00 zilizokuwa zikisambazwa kwenye ATM za Benki ya CRDB.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro ameeleza kuwa baada ya jambazi huyo kujeruhiwa alifariki dunia wakati akiwa njiani kupelekwa hospitali ya taifa Muhimbili.


“Fedha hizo zilikuwa kwenye gari lenye namba za usajili T.155 DGB Nissan mali ya kampuni ya ulinzi ya G4S huku likisindikizwa na askari wawili wa FFU ambao walikuwa kwenye gari lenye namba za usajili T. 997DGQ mali ya G4S lililokuwa likiendeshwa na SOPHIA D/O HUSSEIN,” amesema na kuongeza.


“Aidha katika eneo la tukio kulikuwa na watu wanne waliokuwa kwenye pikipiki mbili aina ya Boxer ambazo hazikusomeka namba na wakati wahudumu wa gari hiyo wakisambaza fedha kwenye ATM ghafla mmoja kati ya watu wale aliruka na kumvamia askari No: G.8925 PC ADAM kwa lengo la kumpora silaha ili kufanikisha zoezi la kupora fedha hizo.” amesema.

Ameeleza kuwa, baada ya kitendo hicho jambazi huyo aliamuriwa asimame lakini alikaidi na ndipo alipigwa risasi iliyomjeruhi mguuni na nyingine tumboni ambapo aliishiwa nguvu na kisha kuwekwa chini ya ulinzi.

Aidha, amesema msako mkali bado unaendelea ili kuwakamata watuhumiwa wengine waliokimbia na pikipiki.

Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro amesema jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa 120 kwa makosa mbalimbali ikiwemo kukutwa na dawa za kulevya

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm limeendelea kufanya misako na oparesheni kali ambapo kuanzia tarehe 09/05/2017 mpaka tarehe 14/05/2017 limefanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 120 kwa makosa mbalimbali ya kiuhalifu. Makosa hayo ni: kupatikana na madawa za kulevya, unyanga’nyi wa kutumia silaha/ nguvu, utapeli, wizi kutoka maungoni, kucheza kamari kuuza pombe haramu ya gongo,kupatikana na bhangi nk katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam,” amesema.

Ameeleza kuwa “Aidha katika oparesheni hii ambayo ni endelevu jumla ya Kete 80 za dawa za kulevya zimekamatwa, huku Puli zikiwa 75,Misokoto ya Bhangi 30 pamoja na pombe haramu ya gongo ipatayo lita 60,

“Oparesheni hii kali ya kuwasaka wahalifu wa makosa hayo mbalimbali ikiwemo kosa la kupatikana na dawa za kulevya ni endelevu na hivyo raia wema wanaombwa kuendelea kutoa ushirikiano mzuri kwa Jeshi la Polisi ili kurahisisha kukamatwa kwa wahalifu hao na hatua kali za kisheria zifuate dhidi yao.”

Amesema Watuhumiwa wote bado wanaendelea kuhojiwa kulingana na makosa yao na pindi upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.
Polisi waua ‘Jambazi’ wakati akijaribu kupora fedha za Benki ya CRDB Polisi waua ‘Jambazi’ wakati akijaribu kupora fedha za Benki ya CRDB Reviewed by Zero Degree on 5/15/2017 10:30:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.