Loading...

Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametoa pole kwa Ruvu Shooting baada ya kupata ajali

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea kwa masikitiko taarifa za kupata ajali kwa msafara wa timu ya Ruvu Shooting FC iliyotokea leo barabara ya Manyoni mkoani Singida wakati kikosi hicho kikitokea Shinyanga kwenda Pwani.

Taarifa kutoka Singida zinasema gari hilo lilipata ajali baada ya kupasuka tairi moja la mbele hivyo kuyumba na kuacha njia eneo la Itigi – kilometa 200 kutoka Singida mjini kuelekea Manyoni hivyo kutoka barabarani kuu kabla ya kugonga mti.

Taarifa hizo zilizothibitishwa na Masau Bwire, zinasema wachezaji watatu akiwamo Bwire mwenyewe ndio waliopata majeraha na kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Singida kwenda kutibiwa. Wachezaji hao ni Yussuf Nguya, Abdul Mpambika na Saidi Dilunga.

Timu hiyo ilikuwa mkoani Shinyanga ilipocheza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2016/17 dhidi ya Stand United na kupoteza kwa mabao 2-1, hata hivyo imebaki kucheza Ligi Kuu ya Vodacom msimu ujao baada ya kushika nafasi ya saba.

Mara baada ya kupata taarifa hizo, Rais wa TFF, Jamal Malinzi mara moja ametuma salamu za kuwapa pole uongozi wa timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania pamoja na timu nzima ya Ruvu Shooting.

“Nawapa pole viongozi wote, makocha na wachezaji. Na kwa wachezaji ambao wamejeruhiwa na viongozi wote waliojeruhiwa akiwamo ndugu yetu Masau Bwire, nawaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka,” amesema Malinzi.

Rais Malinzi alimshukuru Mungu kwa kuepusha vifo kwa wanafamilia hao wa mpira wa miguu hasa wakati huu Watanzania wakiwa makini kufuatilia maendeleo ya timu za taifa.

Taifa Stars – timu ya taifa ya wakubwa inajiandaa kwenda kambini Misri kujiandaa kucheza na Lesotho hapo Juni 10, 2017; Timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ na Serengeti Boys – timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ambayo kwa sasa inapambana kuwania Kombe la Afrika katika fainali zinazofanyika Gabon.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametoa pole kwa Ruvu Shooting baada ya kupata ajali Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametoa pole kwa Ruvu Shooting baada ya kupata ajali Reviewed by Zero Degree on 5/21/2017 11:06:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.