Loading...

Sakata la Escrow laibuka tena Bungeni

MZIMU wa akaunti ya Tegeta Escrow ni miongoni mwa mambo yaliyoibuka bungeni mjini Dodoma jana wakati serikali ilipokumbushwa utekelezaji wa ripoti yake na kuahidi kutoa taarifa ya kina.

Ripoti nyingine zilizokumbushiwa ni pamoja na sakata la Bilioni za Uswisi na pia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ndiye aliyeibua suala hilo wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni, akiitaka serikali kueleza utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu ripoti mbalimbali zikiwamo za uchotwaji wa bilioni za fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow na sakata nyingine zikiwamo za Operesheni Tokomeza na bilioni za Uswisi.

Wakati akijenga hoja yake, Mbowe alisema Bunge ndicho chombo kikuu chenye mamlaka na wajibu wa kuisimamia serikali na kuishauri, akisema hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa Ibara ya 63(2).

"Katika Bunge hili la 10 na mabunge mengine kadhaa, Bunge limekuwa linatoa maazimio kadhaa kuitaka serikali itoe taarifa na serikali imekuwa inaahidi kutoa taarifa… lakini taarifa nyingi ambazo ni maazimio ya Bunge, yamekuwa hayatekelezwi na serikali," alisema.

Aliongeza: "Kwa mfano, kuna maazimio ya Bunge kuhusiana na Operesheni Tokomeza, mpaka leo serikali haijaleta majibu…kuhusu Tegeta Escrow, IPTL mpaka leo haijaleta majibu. Kuna maazimio ya Bunge kuhusu mabilioni ya Uswisi mpaka leo haijaleta majibu na mengine mengi."

Kutokana na hali hiyo, Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Hai, alitaka kujua kauli ya serikali kupitia Waziri Mkuu.

"Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri Mkuu analiambia nini Bunge na analiambia nini taifa kuhusiana na maazimio haya?

"Wewe (Waziri Mkuu) ukiwa kiongozi wa serikali bungeni, utapenda kusema kwamba serikali inalidharau Bunge au serikali haina majibu ya kutoa?" Alihoji Mbowe.

Katika majibu yake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema serikali inaliheshimu Bunge na kuahidi kuwasilisha taarifa bungeni kuhusu utekelezwaji wa maazimio ya chombo hicho cha kutunga sheria.

"Kwanza nataka nikuhakikishie kwamba serikali inaheshimu sana mhimili wa Bunge na inathamini sana maamuzi (uamuzi) ya mhimili huu… na tutaendelea kushirikiana na Bunge katika kupata ushauri na namna nzuri ya kuendesha serikali, kwa mapendekezo ambayo yanatolewa na wabunge kupitia chombo hiki," alisema.

Licha ya majibu hayo, Mbowe alisimama na kuuliza swali la nyongeza, safari hii akitaka serikali iweke wazi tarehe ya kutolewa kwa taarifa hizo za utekelezaji wa maazimio ya Bunge.

"Ni lini (serikali) italeta taarifa hizo za maazimio yaliyopendekezwa na Bunge? Si lazima ilete taarifa kamili ambazo zimeshafanyiwa uchunguzi, bali iingie
kwenye taarifa rasmi za Bunge (hansard) na kuangalia maazimio ambayo yalitolewa na Bunge na kutoa taarifa kwa hatua iliyofikiwa," alisema.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema hawezi kusema ni lini hasa taarifa hizo zitatolewa na serikali, lakini akaliahidi Bunge kuwa watafanya uchambuzi wa maazimio hayo na kuunda kamati mbalimbali ili kutoa majibu yaliyokamilika.

Alisema serikali itaangalia hatua zilizofikiwa kuhusu maazimio hayo na kuziwasilisha bungeni ili wabunge wajue kinachoendelea.

“Matukio ni mengi sana, hivyo yanahitaji kufanyiwa uchambuzi, kuyapitia kwa kina katika uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuunda kamati mbalimbali ili kutoa majibu yaliyokamilika," alisema.

Lilipoibuliwa bungeni wakati wa serikali ya awamu ya nne mwishoni mwa mwaka 2014, sakata la Escrow liliwaponza mawaziri na viongozi katika taasisi mbalimbali ambao walijikuta waking’olewa kwenye nafasi zao, kama ilivyokuwa kwa sakata la ‘Operesheni Tokomeza’ lililowang’oa mawaziri wanne.
Sakata la Escrow laibuka tena Bungeni Sakata la Escrow laibuka tena Bungeni Reviewed by Zero Degree on 5/12/2017 04:18:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.