Loading...

Ujumbe wa beki wa Mbao FC, Yusuph Ndikumana kwa Simba SC

BEKI wa Mbao FC, Yusuph Ndikumana.
BEKI wa Mbao FC, Yusuph Ndikumana, amesema mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania (FA) kati yao na Simba hautabiriki, lakini amewatahadharisha wapinzani wao kuwa watawashangaza.

Akizungumza kabla ya kuingia mjini Dodoma kutakapofanyika mchezo huo, Ndikumana alisema kikosi chao kimepania kushangaza kwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa kwa kuifunga Simba kwenye mchezo huo wa Jumamosi ijayo.

"Mpira ni uwanjani na matokeo yanajulikana baada ya dakika 90..., mchezo utakuwa mgumu, lakini sisi kama Mbao tumejipanga kuhakikisha tunawashangaza Simba na wadau wa mpira kwa kuibuka na ushindi ambao utatuwezesha kushiriki michuano ya kimataifa mwakani," alisema mchezaji huyo ambaye amechangia timu yake kubaki Ligi Kuu msimu huu. 

Aidha, Ndikumana alisema kile walichokifanya kwa Yanga katika michezo yao miwili iliyopita msimu huu ndicho wanachoenda kukifanya Jumamosi mbele ya Simba.

Mbao iliishangaza Yanga kwa kuifunga kwenye mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo kwa bao 1-0 na wakarudia kuiadhibu tena kwenye mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu kwa ushindi kama huo na kujihakikishia kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

Mchezo huo wa fainali ya Kombe la Shirikisho litakalotoa mwakilisha wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, utachezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Credits: Nipashe
Ujumbe wa beki wa Mbao FC, Yusuph Ndikumana kwa Simba SC Ujumbe wa beki wa Mbao FC, Yusuph Ndikumana kwa Simba SC Reviewed by Zero Degree on 5/24/2017 10:43:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.