VIDEO: 'Hat Trick' ya Ronaldo ilivyoiua Atletico jana kwenye nusu fainali ya UEFA
REAL Madrid wameendeleza umwamba kwa wapinzani wao wakubwa Atletico Madrid, baada ya usiku wa kuamkia leo kuwachapa mabao 3-0 kwenye mchezo wa nusu fainali wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, yote yakiwekwa kimiani na Cristiano Ronaldo. Mchezo wa huo ulikuwa unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote kutokana na upinzani wa timu zote, lakini Ronaldo aliendelea kuonyesha umwamba wake.
Kocha wa Atletico, Simeone (kushoto) akisalimiana na Zidane baada ya mchezo. |
Ronaldo alifanikiwa kuifungia timu yake bao la kwanza katika dakika ya kumi ya mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Santiago Bernabeu, kwa kichwa safi baada ya kupata pasi safi toka kwa Casemiro.
Bao hilo lilimfanya Ronaldo aweke rekodi hizo, kwanza lilimfanya kuwa amefunga mabao sita ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika dakika 219 zilizopita, pili lilimfanya awe amefunga mabao 101 kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, yakiwa ni mengi zaidi kuliko timu nzima ya Atletico Madrid ambayo imefunga mabao 100.
Rekodi nyingine iliyowekwa na Ronaldo baada ya kufunga bao hilo ni kwamba lilikuwa bao lake la 50 kwenye michezo ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku akiwa mchezaji wa kwanza kufikisha idadi hiyo na mwisho lilikuwa bao lake la 11 kwenye hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, baada ya Ronaldo kufunga bao hilo, Atletico walijitahidi kupambana kutafuta bao la kusawazisha, lakini ulinzi wa Madrid ambao ulikuwa chini ya Sergio Ramos na Raphael Varane ulifanya kazi kubwa ya kuwazuia. Katika dakika 45 za kwanza Madrid walionekana kutawala baada ya kupiga jumla ya mashuti 11 kuelekea langoni mwa Atletico.
Hata hivyo, wakati wa mapumziko wachezaji wa Atletico Madrid walimvaa mwamuzi Martin Atkinson, wakilalamikia faulo ambayo kipa wa Madrid, Keylor Navas alimchezea mshambuliaji wa Atletico Kévin Gameiro katika dakika ya 29 ya mchezo huo. Kipindi cha pili Atletico walimtoa Gameiro na kumuingiza mshambuliaji hatari, Fernando Torres lakini bado alishindwa kuiokoa timu hiyo na kichapo.
Katika dakika ya 73, Ronaldo alianza kuvunja rekodi zake za kwanza baada ya kufunga bao safi la pili kwa shuti kali akiwa ndani ya eneo la 18 na kuwamaliza nguvu zaidi Atletico. Wakati mashabiki wakianza kutoka uwanjani wakiamini kuwa Ronaldo atafunga mabao hayo mawili tu, hakika staa huyo raia wa Ureno aliamka tena na kuifugia timu yake bao la tatu katika dakika ya 85 baada ya kupata pasi safi toka kwa Luka Modric.
Bao hilo lilikuwa la nane kwa Ronaldo katika michezo mitatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopita , lakini likiwa ni la 52 kwa michezo ya mtoano ya michuano hiyo ikiwa ni hat trick yake ya pili mfululizo baada ya kuwafunga Bayern kwenye robo fainali. Hata hivyo, Jumatano ijayo, Atletico watakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani kuhakikisha wanashinda kwa zaidi ya mabao hayo matatu ili waweze kufuzu hatua ya fainali. Mechi nyingine ya nusu fainali leo ni Juventus ambao watakuwa wageni wa Monaco nchini Ufaransa kuanzia saa 3:45 usiku.
VIDEO: 'Hat Trick' ya Ronaldo ilivyoiua Atletico jana kwenye nusu fainali ya UEFA
Reviewed by Zero Degree
on
5/03/2017 09:41:00 AM
Rating: