Loading...

Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 06


MTUNZI: MC Short Charles Gwimo

Ilipoishia..........Mapigo ya moyo wangu yalianza kurejea katika hali yake ya kawaida huku Mood akiendelea kunicheka sana kana kwamba uso wangu umekuwa kichekesho. Alicheka sana mpaka ushuzi ukamtoka pasina kujijua tena mbele ya watoto warembo kama hao aliokuja nao. Mpaka ninapokuhadithia simulizi hii sijawahi kumshuhudia tena mwanaume aliyejamba Mubashara mbele ya Maghashi bila hata kujali kama alivyofanya jamaa yangu. Niliacha zoezi la kufua kisha nikaanza kupokea utambulisho wa ugeni wa mabinti hao walioambatana na Mood kwa kutajiwa majina yao au wasifu wao kwa ujumla.

Endelea nayo: Utambulisho kwa ugeni huo ulifanywa kwa ufundi na ustadi mkuu kutoka kwa bingwa wa totozi kama nilivyokujuza hapo awali. Huyu si mwingine bali ni Mood mwenyewe kijana shababi kutokea mji kasoro bahari, mji ambao unasadikika kuwa na makabila makuu mawili ambayo ni WALUGURU na WAKAGURU ingawa yapo mengine madogo madogo kama vile wapogoro nk. Inasemekana kuwa kabila la Waluguru lilitokana na jamii hiyo kuwa na makazi yao maeneo ya milimani hasa milima ya Uluguru kwenye maeneo ya MATOMBO na kwingineko. Kimsingi neno luguru hutumiwa sana na makabila yenye asili ya kibantu likimaanisha juu. Kuhusu kabila la Wakaguru nalo pia linasadikika kutokana na mtawala wao wa maeneo ya chini ya milima ya Uluguru yaliyokuwa yakitawaliwa na mtawala aliyekuwa na ulemavu wa mguu mmoja aliokuwa akiutembezea juu juu. Na hicho ndicho chanzo cha kupatikana kwa kabila la “WA - KAGURU”. Najua wazi kuwa msomaji wangu uko kwenye sintofahamu ya mahusiano yaliyopo kati ya Simulizi na makabila hayo ya Waluguru na Wakaguru. Hii imetokana na utambulisho wa binti wa pili aliyeambatana na Fety nilipotambulishwa kuwa ni mmoja kati ya makabila niliyoyazungumzia hapo awali nikimaanisha kuwa yeye ni Mkaguru kwa baba na mama na jina lake halisi ni Fauzia Ayubu au Fey kama walivyokuwa wakimuita marafiki zake. Ashakum Si matusi, kingine kingine kilichonifanya niyazungumzie hayo makabila ni Simulizi niliyowahi kupewa bna rafiki yangu Elisha Magehema akisema kuwa, Zamani zile za utawala wa Kaguru kulitokea ugeni wa Wamisionari wa Kizungu waliofika katika utawala huo kwa lengo la kuihubiri injili. Miongoni mwa zawadi walizokuja nazo zilikuwa ni pamoja na nguo za mitumba za aina mbalimbali zikiwemo chupi. Kichekesho kilikuja katika uvaaji wa chupi kwa watoto wa kike. Watoto wengi wa kike hawakuzipenda chupi eti kwa sababu wazivaapo huwa zinawatekenya na kuwapunguzia hamu ya kushiriki tendo la ndoa wanapofikia umri wa kuolewa na hatimaye wanaume wengi kuoa mke zaidi ya mmoja ili kuipata faraja ya tendo la ndoa. Mpaka leo inasadikika kuwa, mji huo kasoro bahari unaongoza kwa mabinti kutovaa nguo za ndani labda pale tu ambapo mzunguko umepevuka. 


********

Utambulisho ulihitimika kwa mimi kujitambulisha kwa maneno ya uoga huku nikiongeza vitamkwa vya lugha kuashiria kuwa nimeathiriwa na mazingira ya lugha mama. Nilijikaza kisabuni ili na mimi nisionekane mshamba zuzu la kijijini bali mtoto wa kileo ninayekwenda na usasa. Tuligongesheana viganja vya mikono yetu ikiwa ni ishara ya kutambuana. Ujio wa kina Mood haukuwa wa mikono mitupu, bali uliambatana na vifurushi vya aina mbili ambavyo lilikuwa ni begi lililosheheni nguo zilizoletwa kufuliwa na kikapu kikubwa ambacho sikutambua kilikuwa kimebeba vitu gani zaidi ya pua yangu kupokea harufu ya mahanjumati adimu ambayo sikuweza kujua ni aina gani ya chakula kilichosheheneshwa katika kapu hilo. Waliungana na mimi katika zoezi zima la kufua huku Fey akimalizia zangu na Fety akiendelea kufua nguo za Mood. Mnamo saa 7:15 mchana zoezi la kufua nguo kwa wote lilikamilika.

********

Kukamilika kwa zoezi la ufuaji kuliambatana na maandalizi ya msosi ambapo Fety alianza kutuandalia chakula mahususi kwa mchana huo ambapo sikufahamu maandalizi ya msosi huo yalifanyikia wapi na kwa hisani ya nani. Chakula kilicholetwa pale ni pamoja na ndizi za kukaangwa zilizokwenda sambamba na vidari vya kuku na pilau lililopikwa likapikika. Mwendo ulikuwa ni huduma jihudumie mwenyewe. Katika ulaji, katika ulaji hatukukaa pamoja bali tuligawanyika katika makundi mawili yenye watu wawili wawili. Mimi na Fey tulianza kukaa pamoja na Mood na Fety walikaa upande wao. Mimi na Fey tulianza kula kwa kuoneana haya mno na hasa mimi niliyekuwa gulagula au fala katika medani ya mapenzi. Wakati tukiendelea kupata misosi yetu, kwa chati nilitupa wizi ili nione jambo gani wenzetu wanaendelea nalo na kwanini wameamua tukae kwa mtindo wa kutengana. Nilichoweza kubaini ni moja ya mitindo ya kulishana chakula kwa wenzetu mithili ya mapenzi ya njiwa. Nilishuhudia Mood akilishika pande la finyango kwa meno yake na kuanza kumpelekea Fety kwenye kinywa chake huku Fety akiwa amekisubiri kwa muonekano wa kike kike. Nilibaki nimeduwaa kana kwamba sikuwa kwenye msosi mpaka pale niliposhtuliwa kwa sauti ya puani kutoka kwa Fey ikisema, “Devi, mbona unawashangaa wenzako?” Nilijifanya kuonesha hali ya kutokuwa mbali kimawazo kwa kutoa tabasamu lisilo na ladha yoyote kwa wataalamu tu ndilo linafahamika. Fey alikiweka kipande cha kiazi mbata kinywani mwake kisha akaniomba nimsogezee kinywa change. Na mimi bila hiyana nilimsogezea kinywa change huku nikiwa nimeachama kama vile kinda la ndege likisubiri posho kutoka kwa wazazi wake. Ingawa nilihisi kichefuchefu lakini sikupenda nionekane bwege nitozeni mbele ya mtoto Fey. Fey alikileta kipande kile cha kiazi mbatata hadi maeneo ya kinywa change ambapo alipokaribia kinywa changu alikidondosha chini kwa makusudi pasina mimi kutegemea. Ghafla niliupokea ulimi wake na zoezi la kulana denda kwenye ulimi wenye joto la mapenzi likaanza. Kutokana na zoezi hilo eneo langu la siri lilionekana kuvimba kama vile mtu aliyeficha ndizi makojozi kwenye chupi baada ya kuiiba maeneo ya magengeni. Niligutushwa na makofi ya kutupongeza kutoka kwa Fety na Mood jambo lililonifanya nijichomoe mdomoni kwa Fey huku nikiwa na soni za kutosha. Hii haikuwa ni ndoto kama ile niliyokuhadithia bali ni ukweli uliojidhihirisha kujikojolea kwa mara nyingine tena na mkojo ule ule niliojikojolea ndotoni.



********

Siku hiyo ilikuwa ni ya furaha sana kwangu ingawa kwa upande mwingine ilikuwa ni ya maudhi hasa kwa kitendo cha kunyweshana mate eti ni denda. Furaha ilizidi kwa suala zima la ubadilishaji wa mlo kwa siku hiyo vinginevyo ningeungana na wenzangu kwenye kundi letu la wala ugali na maharage kavu kavu. Tulianua nguo zetu tukaagana na wapenzi wetu ingawa mimi sijatamkiwa au kutamka chochote kuhusiana na mapenzi zaidi ya kulishana denda. Ila ninafahamu kuwa matendo katika mapenzi yana nguvu zaidi kuliko maneno. Tuliagana kwa mabusu moto moto huku tukipeana miadi ya kukutana tena maeneo hay ohayo kwa kula bata na kujuana zaidi.

====>>Itaendelea Ijumaa...


Usiikose SEHEMU YA 07>>> ya Riwaya hii ifikapo Ijumaa ya wiki hii, na utaipata hapa Zero Degree pekee.
Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 06 Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 06 Reviewed by Zero Degree on 6/19/2017 02:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.