Loading...

Mlinzi auawa kikatili kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana mkoani Mwanza


Mlinzi mmoja wa maduka ameuawa kwa kukatwakatwa na mapanga na mwingine mmoja kujeruhiwa katika kitongoji cha Sima Majengo, Kata ya Sima Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho Martine Faustine amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutaja jina la mtu aliyepoteza maisha kuwa ni Selemani Buyoga (24) mkazi wa kitongoji cha Sima Majengo na aliyejeruhiwa ni Charles Guli (55) mkazi wa Ngara mkoani Kagera wote wakiwa ni walizi wa kampuni ya ulinzi inayofahamika kwa jina Nyuki ya Kahama Mkoani Shinyanga.

“Mimi taarifa hizo nimezipata saa 11 alfajiri baada ya mama mmoja kuja kwangu na kunieleza nilifika eneo la tukio bila kukawia nikakuta watu wawili mmoja akiwa ameferiki na mwingine amejeruhiwa,” alisema mwenyekiti wa kitongoji cha Sima Majengo.

Nae Mwenyekiti wa kijiji cha Sima, Bahati Petro Mhangwa amewatupia lawama wananchi kwa madai ya kushindwa kutoa taarifa kwa viongozi husika pale wanapopata wageni katika maeneo yao na kuwahifadhi kwa siri na kuwataka waachane na tabia hiyo mara moja.

“Ndungu wanasima kiukweli hii hali inatisha mimi nilitegemea kwamba kwa sasa Sima yetu tupo na amani kumbe sio hivyo jamani nawaombeni tushirikiane kwa pamoja kuwafichua wanafanya vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kuwaleta wageni kwangu ili niwatambue naamini wageni hawa wanaokuja hapa Sima bila taarifa ndiyo wanaosababisha matukio kama haya kutokea,” alisema Mwenyekiti wa kijiji cha Sima.

Diwani wa kata hiyo Makoye Sengerema Lugata amewataka wananchi kujenga desturi ya kutoa taarifa pindi matukio yanapotokea .

“Tukio lilitokea saa saba usiku hadi saa moja wananchi hamjatoa taarifa kwa viongozi na nyinyi viongozi fanyeni hima kufuatilia matukio kama haya wananchi wanatambua pengine hamtoi ushirikiano kwao niwasihi wananchi tushirikiane kwa pamoja kuwafichua waliotekeleza mauaji haya,” alisema Diwani wa kata ya Sima.

Kwa upande wao baadhi ya ndugu wa marehemu na wakazi wa kata hiyo wamesikitishwa na tukio hilo, huku wakiiomba serikali kuimalisha ulinzi katika kata hiyo ili kunusuru mauaji ya mara kwa mara .

“Mimi nasema viongozi wetu hawako makini na kazi yao kwa sababu sisi tunapojitahidi kuwapigia simu kiongozi anakwambia yupo Sengerema kwa namna hii sioni kama tutafika mbali matukio yataendelea kutokea kwa sababu hata ulinzi hapa haujaimarishwa,” walisema Ndugu wa Marehemu.

Jeshi la Polisi limefika katika eneo la tukio na kuuchua mwili wa marehemu na kuupeleka katika Hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema kwenye chumba cha kuhifadhia maiti huku mwingine aliyejeruhiwa akiendelea kupatiwa matibabu.

Kufuatia mauaji haya ya walinzi, kituo hiki kimemtafuta Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama ambae pia ni Mkuu wawila ya ya Sengerema, Emmanuel Kipole ambapo ameyataka makumpuni yote ya ulinzi Wilayani Sengerema yahakikishe yanaajiri walinzi wenye sifa stahiki waliopitia mafunzo ya ulinzi.

“Hakuna anayefurahishwa na matukio haya nitoe rai kwa makampuni yote ya ulinzi wilayani Sengerema yahakikishe yanawakiki walinzi wao kama wanasifa za kuwa walinzi kama hawana waache kazi,” alisema Mkuu wa wilaya.

Matukio ya walinzi kuuawa yameendelea kushika kasi katika Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza ambapo mbali na matukio hayo ya walinzi kutokea katika kata hiyo mapema mwaka jana watu saba wa familia moja walipoteza maisha kwa kukatwa katwa na mapanga na watu wasiofahamika huku chanzo chake kikiwa hakifahamiki.
Mlinzi auawa kikatili kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana mkoani Mwanza Mlinzi auawa kikatili kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana mkoani Mwanza Reviewed by Zero Degree on 6/09/2017 02:19:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.