Loading...

Moto ulivyokatisha maisha ya mmiliki wa 'Shinyanga Guest' jijini Mwanza

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi
MOTO mkubwa uliodumu kwa zaidi ya saa tano, kabla ya kuzimwa na magari ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na gari la maji ya washawasha la Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, umesababisha kifo cha mmiliki wa nyumba ya kulala wageni ya Shinyanga Guest, Maduhu Masunga maarufu kama Mzee Shinyanga.

Moto huo unaodaiwa kuanza kuwaka Juni 10 mwaka huu saa 12:30 jioni kisha kujeruhi watoto wake wawili Ngalula Maduhu, mfanya biashara na mkazi wa mtaa wa Lumumba na Brian Maduhu, uliteketeza mali na vitu vilivyokuwa ndani ya nyumba hiyo ikiwamo kiasi kikubwa cha fedha thamani yake haijafahamika na silaha mbili bastola na bunduki aina ya Shortgun.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema kabla ya ajali hiyo, marehemu alikuwa ndani ya nyumba yake na watoto wake ndipo ghafla moto mkubwa ulipozuka na kuunguza nyumba yake.

“Imedaiwa kufuatia tukio hilo, marehemu Mzee Shinyanga alianza kuchukua baadhi ya mali zake ndani ili kutoka nazo nje, lakini kwa bahati mbaya moto ulizidi kushika kasi na yeye kushindwa kutoka nje na kuungua humo ndani na baadaye kufariki dunia na mali zake kuteketea,” alisema Msangi na kuongeza: 

“Moto huo ungeweza kudhibitiwa mapema, lakini kutokana na miundombinu ya eneo hilo kuwa mibovu, ilishindikana kwani kulikuwa na ukuta mkubwa na kukwamisha magari ya maji ya Jeshi la Zimamoto na Jeshi la Polisikuingia na kusababisha kifo.” 

Katika eneo la tukio, 
moto huo ulishuhudiwa ulivyukua ukiwapa shida askari polisi, askari wa Zimamoto na Uokoaji huku mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wakitoa ushirikiano kudhibiti moto huo ili kuepusha madhara makubwa kwa baadhi ya majengo mengine ya biashara yaliyopo eneo hilo. 

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mwanza, Andrew Mbate, aliwaomba wananchi kuweka miundombinu mizuri ambayo itakuwa rafiki kwenye makazi yao itakayoruhusu uokoaji wa vitu na mali pindi zinapotokea ajali kama hiyo.

“Kwa kweli tumepata shida sana kufanikiwa kuuzima moto huu kutokana na hali halisi ya eneo kushindwa kufikika kutokana na miundombinu husika kuwa mibaya. Tulikosa njia ya kupita kutokana na kuta zilizokuwa zimezungushwa katika nyumba hiyo, hivyo tukapitia kwenye msikiti wa Wahindi ulio jirani,” alisema na kuongeza: 

“Ndipo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Tanesco tuliweza kuudhibiti moto huo na kuepusha madhara makubwa kwa baadhi ya majengo mengine ya biashara yaliyopo eneo hilo.” Jeshi la Polisi pamoja na Zimamoto kwa kushirikiana na Tanesco wanaendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo ili kujua chanzo cha moto huo.
Moto ulivyokatisha maisha ya mmiliki wa 'Shinyanga Guest' jijini Mwanza Moto ulivyokatisha maisha ya mmiliki wa 'Shinyanga Guest' jijini Mwanza Reviewed by Zero Degree on 6/13/2017 02:37:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.