Loading...

Ripoti ya pili ya makinikia yawaweka matatani vigogo watano wa CCM

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ofisi ndogo za chama hicho, Lumumba jijini Dar es Salaam jana.
Ripoti ya kamati ya pili ya makinikia iliyowasilishwa mwanzoni mwa wiki, inawaweka katika wakati mgumu vigogo watano wa CCM, imefahamika.

Ripoti ya kamati hiyo iliyoongozwa na Profesa Nehemiah Osorro ilipendekeza vigogo waliohusika kuingia mikataba mikubwa ya migodi ya madini na kulitia hasara Taifa, wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Kitendo cha Rais John Magufuli kukubali mapendekezo yote 21 ya kamati hiyo, ikiwamo kuwachukulia hatua waliotajwa katika ripoti hiyo, kunafanya uhai wa vigogo hao ndani ya chama tawala kuwa shakani.

“Tutawashughulikia wote, ambaye hataguswa ni marehemu tu,” alisema Magufuli huku akiagiza vyombo vya dola kuanza kuwahoji wote waliotajwa. 

Mbali na kauli hiyo ya Rais, jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alitaka vyombo vya dola viharakishe uchunguzi wao, huku Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku, maarufu kwa jina la Msukuma, akishauri wahusika watimuliwe kutoka chama hicho tawala.

Miongoni mwa vigogo waliotajwa kuhusika kuingia mikataba hiyo ni mawaziri wa zamani wa Wizara ya Nishati na Madini; Dk Abdallah Kigoda (marehemu), Daniel Yona, Nazir Karamagi, William Ngeleja na Profesa Sospeter Muhongo.

Wengine ni wanasheria wakuu wa zamani na manaibu; Andrew Chenge, Johnson Mwanyika, Felix Mrema na Sazi Salula.

Mbali na hao pia wamo makamishna wa madini na wakuu wa idara ya mikataba wa zamani; Paulo Masanja, Ally Samaje, Dk Dalaly Kafumu, Maria Ndossi na Julius Malaba.

Lakini, ambao wanaweza kujikuta matatani ni wale walio kwenye ngazi za uongozi wa chama hicho tawala.

Vigogo hao wanaoweza kuchukuliwa hatua ndani ya chama hicho ni Profesa Muhongo, Karamagi, Ngeleja, Chenge na Kafumu ambao ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na baadhi ni wabunge.

Chenge ni mbunge na mwenyekiti wa Bunge na iwapo ataondolewa CCM atapoteza nafasi yake ya ubunge wa Bariadi Magharibi kama ilivyo kwa wengine wanaoshika nafasi hiyo.

Wabunge hao - Kafumu (Igunga), Profesa Muhongo (Musoma Vijijini) na Ngeleja (Sengerema) - wanaweza kujikuta wakipoteza nafasi za uwakilishi wa wananchi wao bungeni iwapo watavuliwa uanachama.

Karamagi, mfanyabiashara ambaye amewahi kuwa mbunge wa Bukoba Vijijini alishindwa katika mchujo wa chama chake kwenye uchaguzi wa 2010 ikiwa ni miaka miwili tangu ajiuzulu uwaziri wa nishati na madini kutokana na kashfa ya mitambo ya kufua umeme ya Richmond.

Akizungumza Machi 11 kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM mjini Dodoma, Polepole alisema chama hicho hakiwezi kuwavumilia wanachama na viongozi watakaokwenda kinyume na maadili.

“Wanachama na viongozi wa CCM, ambao kwa wakati wowote ule watakwenda kinyume na maadili, watakihujumu Chama cha Mapinduzi, watajihusisha na rushwa, ubadhirifu na tabia zozote zile ambazo kwa asili yake zinakwenda kinyume na uongozi bora na uaminifu, (wataadhibiwa) kuhakikisha chama chetu kinakuwa ni mfano wa vyama vyote sio tu Tanzania, lakini Afrika nzima kwa ujumla,” alisema Polepole. 

Alitoa kauli hiyo alipokuwa akitangaza kuwatimua wanachama 12, wakiwamo wajumbe wawili wa Halmashauri Kuu, wenyeviti wanne wa mikoa, watano wa wilaya na mwenyekiti wa UWT kwa madai ya kukisaliti chama hicho wakati wa Uchaguzi Mkuu 2015.

Waliofukuzwa wakati huo ni pamoja na Sophia Simba, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa UWT na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.

Wenyeviti wa mikoa waliotimuliwa ni Jesca Msambatavangu (Iringa), Ramadhani Madabida (Dar es Salaam), Erasto Kwilasa (Shinyanga) na Christopher Sanya (Mara).

Wajumbe wa Halmashauri Kuu waliofukuzwa uanachama ni Ally Sumaye (Babati Mjini) na Erasto Manga (Arumeru).

Ikiwa ni miezi mitatu tangu CCM ifanye uamuzi huo mgumu, suala hilo linaweza kujirudia tena, lakini safari hii kwa wanachama ambao tuhuma zao hazihusiani moja kwa moja na chama.

Jana, Polepole aliendelea kuwa na msimamo huohuo aliposema chama hicho kinasubiri makada hao wahojiwe na kwamba ikithibitika walihusika watachukuliwa hatua za kinidhamu.

“Tunaomba vyombo vya dola vianze kazi ya kuwahoji watu hao haraka na makada waliotajwa watoe ushirikiano ili ukweli ujulikane ili chama kiwachukulie hatua za kinidhamu,” alisema. 

Alisema chama hicho kinampongeza Rais John Magufuli kwa ujasiri aliounyesha katika kusimamia rasilimali za Watanzania.

“Tunamuunga mkono Rais Magufuli, tuko pamoja naye ameonyesha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano si ya kinyonge,” alisema. 

Alisema Watanzania wanatakiwa kushirikiana katika kipindi hiki kumuunga mkono Rais ili apate nguvu ya kusimamia rasilimali nyingine.

“Wako watu wachache ambao wanataka kumkatisha tamaa, lakini tulio wengi tuendelee kushikamana kumpa moyo Rais wetu,” alisema. 

“Katika Ilani ya CCM, kifungu cha 35 (k) tumeweka wazi kuwa tutarekebisha mfumo wa uendeshaji wa migodi ili kukomesha utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi,” alisema. 

Alisema pamoja na ilani kuahidi hayo, kitendo cha Rais Magufuli kimewapa nguvu Watanzania ya kusimamia rasilimali za nchi.

“Tunaomba aendelee kutuongoza kusimamia madini mengine kama almasi na rasilimali nyingine za nchi,” alisema.
Ripoti ya pili ya makinikia yawaweka matatani vigogo watano wa CCM Ripoti ya pili ya makinikia yawaweka matatani vigogo watano wa CCM Reviewed by Zero Degree on 6/16/2017 08:02:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.