Loading...

TFDA yazuia uuzwaji wa unga wa sembe


MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, imezuia kuuzwa kwa unga wa sembe wa kilo 500 kutoka kwenye Kampuni ya Kahama Family Super Sembe, kwa kile walichodai kuwa bidhaa hiyo haijakaguliwa na mamlaka hiyo.

Pia imezua uuzwaji wa chumvi ambao haujafuata utaratibu ikiwemo kuwekwa kwenye mifuko bila ya kuwa na anuani ya mtengenezaji. Mratibu wa TDFA Wilaya ya Kahama, Kalisto John aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake juu ya baadhi ya wafanyabiashara katika mji huo ambao wamekuwa wakiuza sembe pamoja na chumvi bila ya kufuata maagizo kutoka katika mamlaka zinazosimamia biashara na utengenezaji husika.

John alisema katika wiki mbili zilizopita mamlaka hiyo ilifanya ukaguzi katika baadhi ya maghala yaliyopo katika mji wa Kahama yanayohifadhi vyakula mbalimbali, kubaini kuwa mengi yalikuwa bado hayajapata usajili kutoka katika mamlaka hiyo. Alisema kumekuwa na uanzishwaji wa maghala hayo kila siku bila ya kufuata taratibu katika mamlaka husika hali ambayo imefanya mengi kuzuiliwa kufanya biashara hiyo hadi hapo watakapofuata utaratibu wa kusajili na kukaguliwa na mamlaka hiyo.

“Sisi tukikuta ghala lako la kuhifadhia chakula halijasajiliwa, hatujali hata kama kilicho ndani ni mali halali vyote tunaandika kuwa sio halali kwa matumizi ya binadamu mpaka hapo hatua za kisheria katika kusajili zitakapofuatwa,” alisema katika ghala hilo la Kampuni ya Kahama family Super Sembe ambaye Mmiliki wake ni Lucas Kishimbe, ghala lake lilikuwa halijapata usajili na pia walikuta sampuli za unga huo hazijachukuliwa kwenda kufanyiwa uchunguzi katika mamalaka hiyo ili kuona kama unafaa kwa matumizi ya binadamu.

Kuhusu chumvi, John alisema kumekuwa na bidhaa hiyo ambayo haina anuani, hata utengenezwaji ambayo imekuwa ikiingizwa katika Mji wa Kahama hali ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya watu wakati wa matumizi yake, hivyo mamlaka yake bado inafanya uchunguzi kuhusu suala hilo. Kwa upande wake mmiliki wa Kampuni ya Kahama super Sembe, alisema kampuni yake ipo kihalali na kuongeza kuwa watu hao kutoka TDFA walifika katika ghala lake na kumtaka kuboresha milango kwa kutoa Sh 100,000 na si kumfungia biashara yake.

Mratibu huyo wa TFDA, alisema kuwa katika Mji wa Kahama kuna jumla ya viwanda 180, lakini baadhi yake vimekuwa havina usajili kutoka katika mamlaka hiyo huku vikiendelea kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo unga ambao unaweza kuhatarisha afya za watu.
TFDA yazuia uuzwaji wa unga wa sembe TFDA yazuia uuzwaji wa unga wa sembe Reviewed by Zero Degree on 6/26/2017 03:06:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.