Loading...

Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 13


MTUNZI: MC Short Charles Gwimo

Ilipoishia.........Nikiwa bado naendelea kumminia sifa za kinafiki, Mood alinikata maneno kwa kunitolea malalamishi kutoka kwa Fety, eti kwanini nilimpotezea Fauzia kwa kutoonekana kwenye disko ilihali yeye alikuja ukumbini kunifuata. Sikuwa na majibu ya moja kwa moja zaidi ya kujichekesha kama Malaya aliyekuwa mawindoni aliyebahatisha buzi bwege. Malalamiko hayo yalihitimishwa kwa Mood kunieleza, Fety na Fey wanatusubiria kwa hamu mchana wa siku hiyo maeneo ya bandari ndogo ya Kibirizi kwa ajili ya maongezi zaidi.

Endelea nayo: Mnamo saa sita adhuhuri, tulikuwa njia moja kuelekea maeneo ya kibirizi kwenye mapumziko ya mualiko rasmi kutoka kwa Fety na Fauzia. Nilipigilia modo yangu ya mtumba iliyonitoa chicha mithili ya mmoja wa ‘ma-stage show’ wa bongo fleva. ‘FUBU’ na chini simple boot, raba shingo fupi. Nilijipulizia pafyumu aina ya ‘YU’ iliyonikolea kinoma jambo ambalo lilisababisha watu watubenjulie shingo zao mithili ya feni kwa kutazama kuanzia mwanzo hadi mwisho wa safari yetu, yaani kibirizi. Ungebahatika kutuona siku hiyo usingesita kutuweka kwenye orodha ya watoto wa kishua kutoka familia za mboga saba. Tulishuka kwenye Noah ya kukodi maeneo ya fukwe za kibirizi zilizo maarufu kwa utoaji wa dagaa na migebuka kwa wingi katika Ziwa Tanganyika. Eneo hili si maarufu kwa mapumziko kama uwazavyo bali ni maeneo muhimu kwa upatikanaji wa vitoweo vya viumbe waishio majini. Tulipokewa na shombo ya samaki wabichi na mchino sambamba na nzi kedekede kana kwamba tuko jalalani. Eneo hili la Kibirizi linasadikika kuwa kama kituo kisicho rasmi cha kupokelea wakimbizi kutoka nchi jirani ya DRC.


*******

Tulipokelewa na magashi wetu waliokuwa bomba kwa mavazi yao nadhifu. Wote walivalia ‘mini-skirt za jeans’ zilizowashika maungo barabara kitendo ambacho kiliwaacha wanaume wakware ndani ya majonzi ya kuuguza nyonda. Skirt zao zilikua juu ya magoti na kuyaacha mapaja yao laini ndani ya muonekano wa kuwachanganya wanaume rijali na wale wasio riziki. Tulikaa kwenye moja ya eneo tulivu katika fukwe hii ya kibirizi iliyokuwa imesheheni watu mbalimbali. Tuliagiza vinywaji baridi ili kuzipoza koo zetu zilizokuwa kavu. Tulianza mazungumzo ya kubadilishana mitazamo ya kimapenzi baina ya wavulana na wasichana kwa kuijadili mada isemayo “Wanawake na wanaume ni kundi gani linaloongoza katika usaliti wa kimapenzi?” Katika mada hii hakuna mshindi wa hoja aliyepatikana zaidi ya kila upande kujitetea na kuuponda upande kinzani. Fauzia aliendelea kuipamba mada hiyo ili anichokonoe mimi niliyefanya usaliti wa kumkwepa jana yake. Nilipogundua hilo, kwa haraka sana niliyabadili mazungumzo yetu kutoka mada ya usaliti hadi mada ya kuomba msamaha. Nilimsogeza Fey mapajani mwangu huku nikimkunakuna mgongoni ili atulize munkari wa kuhoji kisichohojika. Nilianza kwa hisia kali, “Fauzia mpenzi, najua jana uliumia sana mara baada ya kunikosa kwenye ukumbi wa disko. Kwa ufupi ni kwamba, nilipoona ninaandamwa na wale madada wageni, sikupenda kujirahisisha kama walivyodhania. Hii yote ilitokana na mapenzi yangu juu yako ulionioneshea siku ya kwanza kabisa ya kuonana kwetu, niliamua kutojionesha ukumbini ili nisiujeruhi moyo wako mbichi wa mapenzi uliotokea kunisukumia damu mimi bila hiyana yoyote, na hii ndiyo sababu ya kutoingia kwenye disko”. Kabla hajajibu chochote niliendelea kumjaza maneno mfululizo na ya faraja, “Fauzia kipenzi, binafsi siwezi kukuchanganya na vidudu mtu au madunganyembe katika penzi letu hili changa ambalo linatakiwa litunzwe na kuheshimiwa pasina kuingiliwa mtu yoyote labda tu Mood na Fety tena kwa ushauri na sio vinginevyo.” Nilipofikia hapo, Mood na Fety walitupigia makofi ya furaha ambayo yaliifanya mioyo yetu kusuuzika. Niliendelea kuumwaga uongo mintarafu ukweli, ilihali ukweli niliujua mwenyewe. Nilimalizia risala yangu ambayo mpaka leo ninavyokumwagia simulizi hii ya ukweli sikumbuki maneno yalinibubujikaje mdomoni mwangu. Yalinitoka kama ifuatavyo, “Fauzia wa ubani, ni rahisi sana kumkanyaga nyoka gizani na ukahisi kuwa ni nyoka lakini sio rahisi kuitambua thamani ya pesa ulioikanyaga gizani, hivyo basi, mimi ni sawa na pesa kwako kwani najua hunipendi wewe tu bali kuna wengine pia. Kwa kuijua thamani yangu kwako nimekudhihirishia mchana kweupe kwa kuukubali mwaliko wenu adhimu wa kuvinjari kwenye ufukwe huu wa bandari ya kibirizi. Neno langu muhimu kwako si lingine zaidi ya lile nililozoezwa kusema nifanyapo kosa lolote yaani namaanisha kuwa ninaomba MSAMAHA”. Fauzia au Fey alisimama kutoka mapajani mwangu huku machozi yakiuzunguka mduara wa macho yake mithili ya mpishi aliyeingiliwa na maji ya vitunguu kwa ghafla. Alinisimamisha kisha akausogeza mdomo wake mkabala na wangu na kuninywesha masazo ya soda yaliyokuwa kinywani mwake huku nikimtegea kinywa changu mithili ya kinda la njiwa manga au tetere. Fauzia alimalizia kwa kusema, “Nimekusamehe devi wangu”

*******
Kwa kuwa jua lilikuwa ni kali kuliko, na joto kuongezeka miilini mwetu, Fety alitushauri tukacheze na maji ya ziwa tuipoze miili yetu. Moyoni niliona kama nimepewa mtihani wa kutolingana na daraja langu kielimu kwani mimi na kuogelea ilikuwa ni sawa na kumtunza samaki nchi kavu. Nilizoea kuogelea kwenye maji yasiyo na hadhi kama hii ya ziwa kwa kuogelea kwenye madimbwi ya Nyamagubwe, nyanga na kashenyi yaliyopo Kabanga kwetu wilayani Kasulu. Nilijikaza kisabuni kwa kutoa mkubalio wa shingo kuonesha kuwa ombi hilo ni sahihi. Kwa kuwa Fety na Fey walilijua hilo la kuogelea kutoka mapema, walikuja wamejiandaa kwa nguo za kuogelea tofauti na sisi. Kwa upande wetu tulivalia nguo za ndaani maarufu kama VIP ambazo zilikuwa ni lulu kwa kipindi hicho. Muundo wa hizo VIP unaweza kushabiana na boxer za kileo sema utofauti ni umalighafi wa matengenezo tu. Kwa upande wao walivalia ‘skin tight’ zilizowashika sawasawa kwa kuisanifu miili yao kama vile walikuwa watupu. Tuliogelea sana huku tukicheza michezo yote ambayo wewe msomaji wangu nahisi haukuwahi kuicheza hata nukta labda utaicheza utakapofanikiwa kwenda sambamba na simulizi hii ya Fumanizi la Mapenzi ndani ya Zero Degree. Tulichoshana kwa michezo mingi jambo lililosababisha hata via vyetu vya uzazi visipendane bali vichukiane pasina hata mgogoro wowote. Tulipotosheka na michezo yetu, tulirudi kwenye maeneo tulipovulia nguo zetu ili tujiandae kwa safari ya kurudi shuleni. Kwa kuwa maeneo hayo yalikuwa na uwazi, Fauzia aliniomba nimsindikize kwenye moja ya boti lililokuwa chakavu ili abadilishe nguo. Tulipofika mule ndani, aliniomba niyafumbe macho yangu ili nisivione visivyoonekana wakati wa mchana labda kwa bahati tu. Wakati akibadili nguo zake. Bila hiyana niliyafumba macho yangu huku nikiangalia pembeni kabissa ili nisishawishike hata kumuangalia. Zilipopita kama dakika nne na ushei niliyafumbua macho yangu nikidhani kuwa Fauzia alikwisha maliza kuvaa. Nilipoyafumbua macho yangu tu SALALAA! Sikuamini nilichokiona kwani Fauzia alikuwa mtupu kama alivyopokelewa na wakunga siku ile ya kuzaliwa kwake. Presha ilinipanda kwa kasi kwani ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kuyaona maumbile kama hayo tena mubashara. Nilipandwa na jinamizi la mapenzi kwa kutaka kumvamia lakini nikayakumbuka maneno ya rafiki yangu Mood yaliyogonga ubongoni mwangu ghafla, “Mapenzi sio ubondia, ili ujilie kwa raha yahitaji kuandaana”.

====>>Itaendelea wiki ijayo...


Usiikose SEHEMU YA 14>>> ya Riwaya hii ifikapo Jumatatu ya wiki ijayo, na utaipata hapa Zero Degree pekee.
Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 13 Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 13 Reviewed by Zero Degree on 7/14/2017 11:04:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.