Loading...

Safari ya Watanzania kuachana na nguo za mitumba imewadia


Waziri Kassim Majaliwa amesema safari ya Watanzania kuachana na nguo za mitumba imewadia kutokana na uwepo wa viwanda vya kutengeneza nguo nchini.

Waziri Mkuu alisema hayo jana wakati alipotembelea kiwanda cha nyuzi cha Namera kilichoko Gongo la Mboto na kiwanda cha nguo cha Nida kilichopo Ubungo Dar es Salaam ambapo alidai viwanda vya kutengeneza nguo nchini ni ushahidi tosha kwamba nchi iko njiani kuondokana na matumizi ya nguo za mitumba kwa kuwa nguo nyingi zitakuwa zinatengenezwa nchini, hivyo kupatikana kwa bei nafuu.

Mbali na hilo Waziri Mkuu aliwapa matumaini wakulima wa pamba na kusema hawana sababu ya kwenda kuuza nje ya nchi na badala yake wauze pamba hiyo katika viwanda vya ndani ili vizalishe nguo za kutosha zitakazouzwa nchini kwa gharama nafuu.

“Pamba yote inaweza kuchakatwa nchini, hivyo hakuna haja ya kuiuza nje ya nchi. Natoa wito kwa wakulima wetu wa pamba walime mazao ya kutosha kwa sababu soko la uhakika lipo na hii ndio safari ya mwisho ya mitumba Tanzania" alisema Waziri Mkuu.

Mbali na hilo Waziri Mkuu alitoa wito kwa wamiliki wa viwanda vyote nchini kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi waishio katika maeneo ya karibu na viwanda hivyo sambamba na kulipa kodi kwa wakati na kwa viwango sahihi.

Kwa mujibu wa Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa Tanzania imeazimia kufikia mwaka 2018 kuachana na biashara ya kuingiza nguo za mitumba kutoka nje, makubaliano ambayo yalifikiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Safari ya Watanzania kuachana na nguo za mitumba imewadia Safari ya Watanzania kuachana na nguo za mitumba imewadia Reviewed by Zero Degree on 7/16/2017 02:06:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.