Loading...

Taifa Stars yatinga nusu fainali COSAFA baada ya kuwafunga mabingwa watetezi, Afrika Kusini


TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars imefanya maajabu kwa kutinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la COSAFA jana kwa kuwafunga mabingwa watetezi na wenyeji wa michuano, timu ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana.

Mshambuliaji Elius Maguli anayekipiga klabu ya Dhofar inayoshiriki Ligi Kuu Oman ndiye aliyefunga bao hilo dakika ya 18 kwa shuti. Taifa Stars sasa itamenyana na Zambia katika mechi ya nusu fainali baada ya Zambia kuitoa Botswana juzi katika robo fainali nyingine.

Baada ya kufungwa bao hilo, Afrika Kusini walibadilika na kufanya mashambulizi mengi katika lango la Tanzania, lakini washambuliaji wao walikosa umakini na kushindwa kufunga. Taifa Stars walirudi nyuma na kujihami huku wakitumia mashambulizi ya kushtukiza, hadi mapumziko hakukuwa na mabadiliko.

Kipindi cha pili, Afrika Kusini waliingia kwa kasi na kulishambulia zaidi lango la Tanzania, lakini washambuliaji wake walipoteza nafasi nyingi. Kocha Salum Mayanga alifanya mabadiliko, dakika ya 49 kwa kumtoa Thomas Ulimwengu na kumuingiza Simon Msuva aliyeonekana kukaa na mpira na kuwasumbua mabeki wa Afrika Kusini.

Afrika Kusini walilisakama lango la Taifa Stars mara kwa mara lakini safu ya ulinzi chini ya nahodha Himid Mao na Erasto Nyoni ilihimili. Kocha wa Stars, Salum Mayanga aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonesha juhudi kubwa uwanjani hata kupata matokeo hayo mazuri.

Alisema wataendelea kucheza kwa nidhamu nusu fainali ili kutimiza lengo lao la kufika fainali na kutwaa ubingwa wa COSAFA. Maguli alichaguliwa mchezaji bora wa mechi hiyo na kukabidhiwa tuzo maalumu. Aliwashukuru mashabiki wa Tanzania waliojitokeza uwanjani hapo kuwashangilia.
Taifa Stars yatinga nusu fainali COSAFA baada ya kuwafunga mabingwa watetezi, Afrika Kusini Taifa Stars yatinga nusu fainali COSAFA baada ya kuwafunga mabingwa watetezi, Afrika Kusini Reviewed by Zero Degree on 7/03/2017 05:02:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.