Loading...

Bei ya mbolea yashushwa nchi nzima

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba
SERIKALI imetangaza neema ya aina yake kwa wakulima nchini kote baada ya kutoa bei elekezi ya mbolea yenye unafuu mkubwa nchini kote.

Katika maelekezo hayo, Serikali imetangaza kuwa bei ya juu zaidi haipaswi kuvuka Sh. 56,000, huku kwa ujumla wake viwango hivyo vikitofautiana kati ya eneo moja na jingine, lengo likiwa ni kuwapa nafuu wakulima na kuongeza ufanisi katika sekta hiyo. 

Aidha, serikali imeitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote watakaokiuka bei elekezi kwa namna waitakayo wao.

Akizungumza na wakulima wa nafaka jijini Mwanza jana, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, alisema kuanzia sasa hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kuuza mbolea hizo kwa bei holela.

Alisema mfuko wa kilogramu 50 wa mbolea ya kupandia kwa bei ya juu ni Sh. 53,000 kwa mikoa ya kanda za Mshariki, Kati na Kaskazini, Sh. 56,000 kwa mikoa mingine.

Waziri huyo alisema kwa mikoa ya kanda ya Magharibi, Ziwa na Nyanda za Juu Kusini, mbolea ya kukuzia kwa mfuko wa kilogramu 50 itauzwa 41,000 hadi 43,000, huku mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Mashariki na Kati itakuwa Sh. 38,000 na 43,000.

Bei hizi ni pungufu kwa asilimia 15 ukilinganisha na bei ya Urea iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh. 45,000 hadi 70,000 kwa mfuko wa kilogramu 50,000, yapo maeneo itapungua hadi asilimia 43,000 kwani kuna maeneo ilifika Sh. 100,000 mfano Tanga, Arusha na kwingine,” alisema na kuongeza

“TRA fuatilieni … mkibaini mtu kauza kwa bei zaidi, huyo ni halali yenu ni mwizi, wakulima mwaka huu wanapunguzo kubwa, tunawataka Wakuu wa mikoa, wilaya, maafisa biashara wasimamie hili na tusisikie mtu yeyote anauza zaidi ya hapo.” 

Kwa mujibu wa Tizeba, “Mbolea ya Urea ya kukuzia na DAP ya kukuzia zitauzwa kwa bei maalum katika maeneo yote ya Tanzania Bara, hakuna kwa kuwa mimi nina duka la pembejeo naweza kuuza kwa bei ninayotaka, wafanyabiashara wa pembejeo wanafahamu makubalinao tuliyokuwa nayo,” alisema na kuongeza:

“Tumeanza mfumo wa uagizaji mbolea kwa pamoja na msharti yaliyomo kwenye kanuni tukishapata bei ya kuagizia tunatangaza bei elekezi kwa ajili ya aina zilizoingizwa chini ya mfumo huo alafu tunatangaza bei elekezi.” 

Alisema serikali inahakikisha viwanda vinavyojengwa ni vyenye mnyororo wa thamani kwa kuhakikisha malighafi inapatikana kwa wakati.

“Moja ya mambo yaliyofanya kilimo kisikuwe kwa haraka upatikanaji wa pembejeo ambazo ni mbegu, dawa na mbolea, tumekuwa na tatizo kwa muda mrefu. Tanzania utoshelevu wa mbegu bora ni asilimia 35, asilimia 65 ni mbegu inayoagizwa na wafanyabiashara kutoka nje,” alisema na kuongeza: 

“Sasa hivi tuna mpango maalum na kwa kushirikiana na bilionea Bill Gate ambaye atatoa fedha kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa mbolea nchini, wataalamu wake watafika mwishoni mwa mwezi huu, watakaa na wataalamu wetu na kutengeneza mfumo utakaohusisha serikali na wafanyabishara wa uzalishaji wa mbegu.” 

Dk. Tizeba ambaye pia ni Mbunge wa Buchosa, alisema wanafanya hivyo ili kujitosheleza kwa mbegu bora, hasa za mazao makuu ya chakula na biashara, huku akitolea mfano wa zao la pamba ambalo kwa msimu huu Mwanza itazalisha tani 20,000 kutoka tani 6,000 walizozalisha msimu uliopita.

“Pragramu ya mbegu kufikia 2019 kutakuwa utoshelevu wa mbegu bora ya pamba aina ya UKM08,” alisema. 

Awali, Mbunge wa Viti Maalum mkoani Mwanza, Kiteto Koshuma, alisema kilio kikubwa kwa wakulima ni kupata mbegu bora.

“Tunaiomba serikali kulisimamia suala hili kwa kuwa bila mbegu bora hakuna kilimo, hakuna mazao na hakuna mavuno kwa ajili ya viwanda, na ajira zitakosekana, hivyo suala hili linahitaji usimamizi thabiti,” alisema.
Bei ya mbolea yashushwa nchi nzima Bei ya mbolea yashushwa nchi nzima Reviewed by Zero Degree on 8/19/2017 10:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.