Loading...

Kiini cha mauaji Kibiti chaanikwa

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali IGP) Simon Sirro
BAADA ya sintofahamu ya miaka miwili ya mauaji ya watu katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani, hatimaye Jeshi la Polisi limefunguka na kueleza kiini chake.

Watu 40, wakiwamo askari polisi 15, wameripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi katika wilaya hizo tangu mauaji hayo, yalipoanza mwaka 2015.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali IGP) Simon Sirro, katika mahojiano maalum na kituo cha Radio One yaliyorushwa kwenye kipindi chake cha 'Kumepambazuka' jana asubuhi, alisema uchunguzi wao umebaini wauaji walikuwa wanalipa kisasi kwa kile alichodai hisia za kutotendewa haki na baadhi ya watendaji wa serikali na maofisa wa jeshi hilo.

IGP Sirro alisema imechukua muda mrefu kwa jeshi hilo, kukabiliana na wahusika wa mauaji hayo kutokana na wauaji kujipenyeza ndani ya jamii ya wilaya hizo kwa karibu muongo mmoja, hivyo kuwa sehemu ya wakazi maeneo husika.

"Waliingia kwenye maeneo hayo (Kibiti, Mkuranga na Rufiji) miaka nane kabla ya kuanza mauaji," IGP Sirro alisema. "Walijipenyeza kwa njia mbalimbali ... unadhani wanaendesha mafunzo ya kidini kumbe kinachofanyika ni mambo tofauti kabisa." 

"(Wauaji) waliwapotosha watu kwamba 'elimu mnayopewa hii haina maana'. Wakafundisha karate, judo na namna ya kutumia silaha." 

Alisema operesheni ilivyofanywa kwenye maeneo husika imefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa kadhaa wa mauaji hayo, lakini baadhi yao wamekimbilia maeneo mengine ya nchi.

Aliwataka viongozi wote wa kamati za ulinzi na usalama kuanzia ngazi ya mtaa, wahakikishe wanatoa taarifa za kuwafichua wahusika wa matukio hayo katika maeneo yao, akibainisha kuwa mara nyingi wamekuwa wakinunua maeneo makubwa na kuyatumia kwa mafunzo yao kwa siri.

Katika mahojiano hayo, IGP Sirro alisema uchunguzi wao umebaini kikundi hicho hakina sifa za kigaidi isipokuwa "ni cha kijambazi tu".

Baadhi ya watu waliouawa katika wilaya hizo za mkoa wa Pwani ni pamoja na Ramadhani Mzuzuri (45), mkazi wa Ruaruke wilayani Kibiti aliyeuawa kwa kupigwa risasi nane nyumbani kwake usiku wa kuamkia Julai 10, mwaka huu huku wauaji wakimjeruhi pia mke wake, Halima Mzururi kwa kumpiga risasi tatu.

Usiku wa kuamkia Juni 28, mwaka huu, viongozi wawili wilaya hiyo waliuawa na kundi hilo kwa kupigwa risasi. Waliouawa siku hiyo ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mangwi, Maiko Nicholaus na Mtendaji wa Kijiji cha Mangwi kilichopo Kata ya Mchukwi wilayani humo. Katika tukio hilo, wauaji pia walichoma moto nyumba za viongozi hao.

Mauaji hayo yalitokea ikiwa ni wiki moja tangu kuuawa kwa kupigwa risasi kwa askari wawili wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakiwa kazini katika kijiji cha Msafiri, Kata ya Bungu wilayani humo.

Mbali ya kuwaua askari hao, wauaji walichoma moto gari na pikipiki vya askari hao.

Mei mwaka jana, matukio matatu yalitokea ambayo ni pamoja na kuuawa kwa kupigwa risasi kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunga, Saidi Mbwana.

Oktoba aliuawa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyambuga, Ally Milandu baada ya kuvamiwa na watu wanne waliomshambulia kwa kumpiga risasi.

Novemba wenyeviti wawili wa vitongoji vya kijiji cha Nyambunda waliuawa kwa kupigwa risasi kabla ya kuuawa kwa mfanyabiashara Oswald Mrope kwa kupigwa risasi mbele ya familia yake katika kitongoji cha Mkwandara kilichopo kijiji cha Nyambunga Januari mwaka huu.

Februari yalitokea matukio mawili, la kwanza likihusisha majambazi waliovamia nyumba ya mwenyekiti wa kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga ambaye alifanikiwa kutoroka, lakini wahalifu hao walirejea na kuimwagia mafuta nyumba yake na kuichoma moto.

Tukio la pili katika mwezi huo ni la mauaji ya Ofisa Upelelezi wa Wilaya ya Kibiti (OC-CID), Peter Kubezya na Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji Mapato ya Ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na mlinzi Rashid Mgamba ambao waliuawa kwa kupigwa risasi.

Machi Jeshi la Polisi liliwaua watu watatu katika Daraja la Mkapa walipojaribu kukwepa vizuizi vitatu va barabara wakiwa na pikipiki likiwatuhumu kuwa sehemu ya kikundi kinachoendesha mauaji hayo.

Aprili, askari nane waliokuwa kwenye gari la polisi wakitoka kubadilishana lindo na wenzao walishambuliwa na majambazi na saba waliuawa kwa risasi huku mmoja akijeruhiwa, katika eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa wilayani Kibiti.

GENGE LA WAUAJI

Mei viongozi wawili; kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Amir Chanjale na aliyekuwa katibu wa chama hicho, Kata ya Bungu wilayani Kibiti, Arife Mtulia waliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Agosti 10 IGP Sirro alitangaza jeshi hilo, kuwaua watuhumiwa 13 wa genge la mauaji katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji.

Waliouawa, alisema, ni Hassani Ali Njame, Abdallah Abdallah Mbindimbi maarufu kama Abajani, Saidi Abdallah Kilindo, Abdulshakuru Mohamed Ubuguyu, Issa Mohamed Mseketu maarufu kama Mtawa, Rajabu Thomas au Roja na Mohamed Ally Kadude maarufu kama Upolo.

Taarifa ya Sirro ilisema miili sita iliyobaki haikuweza kutambulika mara moja.

Taarifa pia, iliwataja watuhumiwa wanaotafutwa kuwa ni Anafi Rashid Kapelo aka Abuu Mariam, Hassan Haruna Kyakalewa aka Abuu Salma aka Shujaa aka Dokta, Haji Ulatule, Shekhe Hassan Nasri Mzuzuri na Rashid Mtutula.

Kabla ya mafanikio hayo, bingo ya Sh. milioni 10 ilitangazwa na IGP Sirro, kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa wahusika wa mauaji hayo.

Kabla ya bingo ya IGP, Polisi mkoa wa Pwani ilikuwa imetangaza zawadi ya Sh. milioni tano kwa mwananchi yeyote ambaye atafanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa 12 ambao lilidai hujihusisha na mtandao wa mauaji hayo.

IGP Sirro alitangaza dau hilo la Sh. milioni 10 katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari Mei 31, jijini Dar es Salaam.

Alisema kwa yoyote atakayetoa taarifa sahihi ambazo zitawezesha kukamata wahusika wa mauaji ya kinyama dhidi ya raia na askari katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani, atapatiwa fedha hizo.

Source: Nipashe
Kiini cha mauaji Kibiti chaanikwa Kiini cha mauaji Kibiti chaanikwa Reviewed by Zero Degree on 8/24/2017 10:01:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.