Loading...

Maandamano ya kumuombea Tundu Lissu yazuiliwa

Kamanda wa Kanda Maalum ya Kipolisi ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limepiga marufuku maandamo yaliyopangwa kufanywa na Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) ili kumuombea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa alisema yapo maeneo maalumu ya kufanya ibada hivyo ni muhimu wakayatumia hayo na si vinginevyo.

“Nilipokea barua ya BAVICHA wakiomba kibali cha kufanya maandamano hayo lakini nimeshawajibu kwamba hilo haliruhusiwi badala yake watumie makanisa au misikiti, kutimiza azma yao na si vinginevyo, wakitaka wanaweza hata kukesha kwenye maeneo hayo,” alisema.

Kamanda Mambosasa alisema hajapiga marufuku wao kufanya maombi hayo, ila ni vyema wakakutana kanisani au msikitini na si kufanya maandamano kama walivyoomba. Mambosasa alisema polisi ina jukumu la kulinda amani na utulivu, hivyo ikitokea jambo lolote la kuashiria uvunjifu wa amani ni jukumu lao kuzuia hilo, aliongeza kuwa yapo maneno yanayoendelea katika mitandao ya kijamii yenye viashiria vya uvunjifu wa amani.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA, Patrick ole Sosopi aliongea na waandishi wa habari na kueleza azma yao ya kuwakutanisha wanachama wao mbalimbali wa imani tofauti kwa ajili ya kufanya maombezi ya kitaifa, kumuombea Mbunge Lissu.

Sosopi alisema jambo hilo halihusiani na mambo ya kisiasa, bali wameamua kukutana kwa lengo la kuombea taifa katika mambo mbalimbali ikiwa pamoja na kuliombea Jeshi la Polisi ili wafanye kazi zao kwa kufuata misingi ya haki na usalama zaidi.

Aidha Mambosasa alipiga marufuku maandamano, yaliyopangwa kufanywa kuanzia Kimara jijini Dar es Salaam na wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa dhumuni la kuwapokea wabunge wao walioapishwa hivi karibuni mjini Dodoma.

“Ni vema kujijengea utamaduni wa kutii sheria bila shuruti hivyo hakuna maandamano yoyote yatakayofanywa kama wana nia ya kuwapokea wafanye bila maandamo,” alisema. 

Katika tukio jingine, Kamanda Mambosasa alisema majira ya saa tatu usiku huko maeneo ya Kwa Mbiku Chamazi, polisi walifanikiwa kukamata silaha moja bastola aina ya Berreta yenye namba A065775Z ikiwa na risasi tano ndani ya magazini katika majibizano ya risasi kati ya askari polisi na majambazi wapatao watano.

Mambosasa alisema silaha hiyo ilipatikana baada askari kupata taarifa ya kuwepo kwa njama za majambazi hao, kufanya uporaji katika maduka ya M-Pesa/ Tigopesa eneo hilo, na hatimaye kuweka mtego ambapo askari walifanikiwa kuwaona majambazi hao wakishuka kwenye gari yao kwa ajili ya kufanya tukio hilo.

“Baada ya majambazi hao kufika eneo la tukio na kugundua kuwa wanafuatiliwa na askari walianza kufyatua risasi kuwashambulia askari na ndipo askari walijibu mashambulizi na kufanikiwa kuwajeruhi majambazi watatu kati ya watano huku wengine wawili wakikimbia,” alisema Mambosasa.

Aliongeza kuwa silaha hiyo ilipopekuliwa kati ya risasi tano zilizokuwa ndani ya magazini moja ilikuwa chemba tayari kwa kutoka huku maganda sita ya silaha hiyo yakipatikana eneo la tukio.

Majambazi waliojeruhiwa walifariki dunia baada ya kufikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kupatiwa matibabu. Msako mkali unaendelea kuwatafuta majambazi wawili waliokimbia
Maandamano ya kumuombea Tundu Lissu yazuiliwa Maandamano ya kumuombea Tundu Lissu yazuiliwa Reviewed by Zero Degree on 9/16/2017 11:34:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.