Loading...

Mashabiki wa Yanga wamgeuzia kibao Mzee Akilimali


Baada ya kuripotiwa mgomo wa mazoezi kwa siku moja uliofanywa na wachezaji wa Yanga, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Klabu ya Yanga, Ibrahim Akilimali ameuhusisha mgomo huo na aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji huku akitaka uchaguzi mkuu wa klabu hiyo ufanyike haraka ili kuweka mambo sawa.

Kauli hiyo imesababisha mzee Akilimali kushambuliwa kwa nguvu kubwa mitandaoni huku wengi wakionekana kumpinga.

Wengi wamesisitiza kuwa Akilimali amekuwa akiwarudisha nyuma na kuibuka wakati wa migogoro.

Wengi wamesema, amekuwa akimshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji baada ya kumfungia mianya ya kupata "chochote".

Lakini Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga naye ana mfumo wa usimamizi mzuri wa fedha, jambo linalomkwaza mzee huyo.

Jumanne ya wiki hii, wachezaji wa Yanga waligomea mazoezi ya timu hiyo yaliyopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda FC utakaopigwa kesho Jumamosi uwanjani hapo.

Mgomo huo ulihusishwa na madai ya wachezaji hao kutolipwa mishahara yao ya miezi miwili.

Kwa mujibu wa taarifa ya Gazeti la CHAMPIONI, Akilimali alisema kuwa, anashangazwa na mgomo wa wachezaji hao na kudai kuwa lazima kuna shinikizo kutoka kwa mtu fulani ambaye anahitaji kitu kwani muda wanaodai ni mdogo, hivyo amemtaka Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga aachane na klabu hiyo na badala yake wafanye uchaguzi wa haraka ili watetee ubingwa wao.

“Nashangazwa kwa kusikia habari ya wachezaji kugoma kwani kwa mujibu wa msemaji wachezaji hao wanadai mshahara wa mwezi mmoja na huu wa tisa ambao bado haujaisha, hivyo itakuwa miwili.

“Napatwa na mashaka katika hilo, kwani inaonyesha wazi kuwa kuna shinikizo kutoka kwa mtu fulani, juzi (Jumatatu ya wiki hii) niliangalia taarifa ya habari kwenye luninga niliwaona viongozi wa benchi la ufundi la Yanga walikwenda kumpa pole aliyekuwa mwenyekiti wetu, japokuwa si vibaya, lakini nina hofu.

“Pia nilimuona (Manji) amekaa muda mwingi na Cannavaro (Nadir Haroub) na aliondoka naye pale mahakamani lakini aliporejea na kuulizwa amezungumza nini na mwenyekiti huyo wa zamani alikataa kusema na badala yake akahitaji kuzungumza na wachezaji wenzake, kisha asubuhi yake ndiyo tunasikia wachezaji wamegoma, siyo bure kuna kitu.

“Huu mgomo kuna shinikizo la mtu fulani, Manji aliondoka mwenyewe Yanga na wala hakufukuzwa aliandika barua na kuiwasilisha klabuni na hata TFF.

“Hatuwezi kuendesha klabu kwa kumtegemea mtu mmoja, mfano alikuwa pembeni miezi mitatu lakini kila kitu kilikwenda vizuri, hivyo ninachokiomba hivi sasa bwana Sanga ambaye ndiye kiongozi wetu kwa sasa na yeye ang’atuke akae pembeni kwa ajili ya kufanya uchaguzi kwa kushirikiana ili tuweze kupata viongozi wapya wa kuendesha klabu.

“Ni vyema tukajipanga hivi sasa kabla ya kufika huko mbele ambapo tunaweza kufeli, ni vyema tukajipanga katika mechi hizi hizi za awali ili tuweze kutetea ubingwa wetu kwa mara ya nne na tuweze kuweka historia ya kuwa mabingwa mara nne mfululizo.

“Sanga inabidi akae pembeni kwa kuwa alishaonyesha woga tangu hapo nyuma, kwamba hawezi kufanya kazi bila ya kuwepo Manji hivyo na yeye aondoke atuachie nafasi lakini tushirikiane kwenye uchaguzi naamini kuna watu wanaweza kuiongoza klabu yetu,” alisema Akilimali.

Source: Champion
Mashabiki wa Yanga wamgeuzia kibao Mzee Akilimali Mashabiki wa Yanga wamgeuzia kibao Mzee Akilimali Reviewed by Zero Degree on 9/23/2017 12:06:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.