Loading...

Polisi yazuia ibada ya kumuombea Tundu Lissu


CHADEMA Mkoani Rukwa kimeshindwa kufanya ibada ya maombi kwa ajili ya Mwanasheria Mkuu wa Chama chao, Mh. Tundu Lissu aliyejeruhiwa kwa risasi hivi karibuni baada ya polisi mkoani humo kuzuia ibada hiyo kwa kudai ni mkusanyiko usio halali.

Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa huo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa kanda, Sadrick Malila amesema wamesikitishwa sana na hatua ya jeshi hilo kwani suala la kumuombea mbunge huyo kamwe lisingeweza kusababisha uvunjifu wa amani ndiyo maana alichukua hatua za kuomba kibali kwa Kamanda wa polisi mkoa huo siku moja kabla.

Amesema kuwa CHADEMA mkoa ilikuwa imewaalika viongozi wa dini kutoka makanisa mbalimbali na wachungaji walikuwa tayari wamejiandaa kwaajili ya maombi hayo, lakini wamelazimika kusitisha baada ya Kamanda wa Polisi, George Kyando kuwaeleza kwamba wasitishe.

"Jana nilimpigia simu Kamanda wa Polisi na kumpa taarifa kwamba leo hapa ofisini tungekuwa na ibada fupi ya kumuombea kiongozi wetu aweze kupata nafuu haraka ili aweze kurejea kwenye majukumu yake na akawa ametukubalia, lakini cha kusikitisha zaidi leo tukiwa tunajiandaa na ibada hiyo na viongozi wakiwa wameshawasili RPC akanipigia na kunijulisha tusitishe zoezi hilo. Inaumiza sana kwani zoezi halikuwa la kisiasa" amesema.

Aidha baada ya zuio hilo Mwenyekiti huyo amelaani shambulio la Mwanasheria wao na kulitaka jeshi la polisi limalize haraka uchunguzi na kuwatia mbaroni walioshughulika na tukio hilo pamoja na wale waliomjeruhi ofisa wa jeshi kwa kumpiga risasi juzi jijini Dar es Salaam ili kukomesha vitendo hivyo.

Malila pia aliwatangazia wanachama wa CHADEMA na wananchi wengine waliokuwa na nia ya kumuombea Lissu kuwa kila mtu afanye maombi binafsi kwani anaamini Mungu ni mwema na atajibu maombi yao.

"Naliomba sana jeshi la polisi kama wameshindwa kulinda raia na mali zao, basi waache kulinda mali watalinda wananchi wenyewe wao wawalinde raia tu kwa kuwa inawezekana majukumu yamewazidia wabaki na kitu kimoja na wanachi wawasaidie kitu kingine. Jana wamezuia vjana wetu Dodoma wasichangie damu wakati hospitali haina damu na hatujui wana maanisha nini." ameongeza.

Naye Katibu wa Baraza la Vijana CHADEMA, Julius Mwita amethibitisha kutokea kwa zuio hilo ambapo amesema kuwa " Hawakuwa wanafanya mkutano wa siasa bali ni ibada maalumu ndiyo maana hata viongozi wa dini wakaalikwa. Tunasikitika wameshindwa kufanikisha kutimiza ibada hiyo kutokana na zuio la polisi".
Polisi yazuia ibada ya kumuombea Tundu Lissu Polisi yazuia ibada ya kumuombea Tundu Lissu Reviewed by Zero Degree on 9/13/2017 07:28:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.