Loading...

Serikali kuboresha maisha ya wastaafu


Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mifumo ya kukusanya mapato pamoja na kuboresha miundombinu ya kiuchumi na kijamii ili kuleta unafuu wa maisha ya Wastaafu na wananchi.

Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mtambile Mhe. Masoud Abdallah Salim (CUF), aliyetaka kujua mpango wa Serikali katika kuboresha mafao ya uzeeni ili kuondoa malalamiko ya hali ngumu ya maisha wanayoishi Wastaafu.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, Serikali kwa sasa imejielekeza zaidi katika kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, nishati ya umeme, maji, huduma za afya, elimu na kiuchumi hususani katika ukusanyaji mapato kwa lengo la kuboresha maisha ya Wastaafu na Wananchi kwa ujumla.

“Tuendelee kuiunga mkono Serikali yetu katika juhudi zake za kujenga uchumi imara, uchumi wa viwanda ambao ndio msingi mkuu wa kuimarisha mapato ya Serikali”. Alisema Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa maboresho ya viwango vya pensheni kwa wastaafu yasiyoendana na maboresho ya miundombinu ya kiuchumi na huduma za kijamii hayawezi kuondoa malalamiko ya Wastaafu hivyo Serikali imelenga zaidi kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii ili kupunguza malalamiko hayo.

Dkt. Kijaji alifafanua kuwa nyongeza ya pensheni kwa Wastaafu, mishahara na maslahi mazuri kwa Watumishi wa Umma itaongezeka kama mikakati na azma ya Serikali ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi itafanikishwa.
Serikali kuboresha maisha ya wastaafu Serikali kuboresha maisha ya wastaafu Reviewed by Zero Degree on 9/08/2017 06:15:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.