Loading...

Tamko la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kufuatia tukio la Tundu Lissu kupigwa risasi

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Bahame Tom Nyanduga
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesitushwa na kusikitishwa na kitendo cha Mhe. Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika kupigwa risasi, tukio lililotokea Septemba 7, 2017 mjini Dodoma.

Tume inalaani vikali kitendo hicho kwani ni kitendo cha uvunjifu mkubwa wa sheria na haki za binadamu.

Tukio hili ambalo limekuja siku chache tu baada ya tukio la ofisi za wanasheria wa IMMMA zilizoko jijini Dar es Salaam kulipuliwa kwa bomu siyo la kawaida, na limeleta hofu siyo kwa familia ya Mhe. Tundu Lissu pekee, bali kwa wananchi wengi nchini.

Isitoshe, matukio haya hayaleti picha nzuri kwa nchi inayoheshimu demokrasia, haki za binadamu na utawala bora.

Hivyo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora:
  1. Inalitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linakamilisha haraka upelelezi wa tukio hilo na kuwapeleka wahusika katika vyombo vya sheria.
    Tume inaamini kuwa iwapo wahusika wa tukio hili watachukuliwa hatua kali itasaidia kukomesha vitendo vya aina hii vinavyofanywa na makundi ya watu wanaojichukulia sheria mkononi ambayo yanaonekana kujitokeza hivi karibuni.
  2. Aidha, inapenda kukumbusha kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora na kuepuka ukiukwaji wa Katiba na sheria za nchi.
  3. Mwisho, inamtakia Mhe. Tundu Lissu kila la kheri katika matibabu yake ili apone haraka.
Imetolewa na:
Mhe. Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Septemba 8, 2017
Tamko la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kufuatia tukio la Tundu Lissu kupigwa risasi Tamko la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kufuatia tukio la Tundu Lissu kupigwa risasi Reviewed by Zero Degree on 9/08/2017 08:56:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.