Loading...

Vigogo waliokamatwa na mzigo wa almasi wafikishwa Kisutu

Shehena ya Almasi iliokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa  Julius Nyerere jijini Dar es Salaam  hivi karibuni. Ambayo jana  ilioyeshwa hadharani wakati Waziri wa  Fedha na Mipango, Dk  Philip Mpango na viongozi wegine wa Serikali,   alipokwenda kukabidhiwa ripoti  ya uchunguzi kuhusu  utoroshwaji wa madini hayo kiwanjani hapo jana (Picha na Ikulu)
MKURUGENZI wa Tathmini, Archard Kalugendo na Mthamini wa Madini, Edward Rweyemamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 2.4.

Kalugendo ambaye ni mkazi wa Kinyerezi huku Rweyemamu mkazi wa Mwananyamala, wamefikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage. Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi alidai kati ya Agosti 25 na 31, mwaka huu maeneo ya Dar es Salaam na Shinyanga, wakiwa watathmini wa serikali walisababisha hasara ya Dola za Marekani 1,118,291.43 sawa na Sh 2,486,396,982.

Kadushi alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika lakini uko mbioni kukamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. Hakimu Mwijage alisema washitakiwa hawatakiwi kujibu chochote hadi Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) atakapoamua shauri hilo liendelee mahakamani hapo au la.

Alisema kwa mujibu wa sheria, kiasi kilichotajwa katika mashitaka hayo ya uhujumu uchumi, mahakama hiyo itasoma mashitaka pekee na kwamba washitakiwa hawatatakiwa kujibu chochote.

Pia alisema masuala ya dhamana, sheria kama zilivyo inafikiriwa na Mahakama Kuu, hivyo mawakili wafuatilie kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana. Wakili wa utetezi, Ludovick Nickson alidai wanaomba upelelezi ukamilishwe na kwamba wapewe tarehe ya karibu ili waombe dhamana Mahakama Kuu.

Wakili Nehemiah Nkoko alidai washitakiwa wamekaa wiki mbili tangu walipokamatwa na kama upelelezi umefanyika mkubwa na sehemu iliyobaki ni ndogo, hivyo wanaomba upelelezi ukamilike haraka. Akijibu hoja hizo, Kadushi alidai watahakikisha upelelezi katika kesi hiyo unakamilika kwa wakati.

Hata hivyo, Hakimu Mwijage alisema upelelezi ukamilike ili mwenye hatia afungwe na asiye na hatia aachiwe. Aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 29, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa
Vigogo waliokamatwa na mzigo wa almasi wafikishwa Kisutu Vigogo waliokamatwa na mzigo wa almasi wafikishwa Kisutu Reviewed by Zero Degree on 9/16/2017 12:23:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.