Loading...

Polisi waliopiga raia Ukonga kuchukuliwa hatua

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa
JESHI la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, litawachukulia hatua kali maofi sa wake watakaobainika kushiriki kushambulia raia katika eneo la Ukonga.

Limesema kuwa tayari limefungua jalada kuhusu tukio hilo na kuwataka wananchi walioshambuliwa kujitokeza. Kauli hiyo ilitolewa jana jijini hapa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa wakati akizungumza na waandishi kuhusu tukio hilo.

Alisema kabla ya wananchi kulalamika kushambuliwa na polisi Oktoba 21 mwaka huu katika maeneo ya kambi ya polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia Ukonga Makao Makuu Mkoa wa Kipolisi Ilala, askari wakiwa kazini walikuta mwili wa askari mwenye namba X-G 475 PC Charles Yanga, ambaye kwa sasa ni marehemu ukiwa pembeni mwa uzio wa kambi hiyo, akiwa ameanguka chini huku pikipiki yake aliyokuwa akiendesha, ikiwa inawaka taa za tahadhari (hazards).

Aliongeza kuwa mwili huo ulikutwa ukiwa na majeraha kwenye paji la uso na sikio moja likiwa limekatwa kabisa. Alisema katika ufuatiliaji, polisi wamebaini askari huyo aliuawa na watu wasiojulikana, kisha kutelekezwa katika maeneo hayo ya kambi ya Polisi.

“Polisi kupitia kikosi kazi chake inaendelea na msako mkali wa ufuatiliaji wa tukio hilo la kinyama ili kuwabaini watuhumiwa waliohusika kutekeleza mauaji hayo na kufikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka yanayowakabili,” alisema Mambosasa.

Alisema baada ya tukio hilo, Oktoba 22 mwaka huu jeshi lilipokea malalamiko ya watu wanaosemekana ni askari kufanya msako na kuwapiga wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na kambi ya Polisi kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) ambao hawana hatia yoyote.

Kamanda Mambosasa alisema katika malalamiko hayo, wananchi walidai kushambuliwa, wanawake kudhalilishwa na watu hao wanaodaiwa kuwa ni polisi. “Jeshi la polisi linalaani vikali vitendo hivyo ambavyo havina maadili ya kazi za Polisi na jalada tayari limefunguliwa na uchunguzi unaendelea ili kuwabaini watuhumiwa wa tukio hilo, tunaomba wananchi watoe ushirikiano kutoa taarifa za wahusika ili kuwachukulia hatua watu au askari waliohusika na matukio hayo ya kuwapiga wananchi, kitendo ambacho ni kinyume na sheria za nchi,” alisema.

Aliongeza kuwa endapo uchunguzi utabaini kuwa waliohusika na matukio hayo ni polisi, basi watakuwa wamekwenda kinyume na viapo vyao, hivyo watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kijeshi na kama watabainika wamehusika na matukio ya unyanyasaji, watashtakiwa kama watu wengine wanavyoshtakiwa.

“Tayari nimekwenda FFU na tumefanya kikao na nimewaambia tukibaini ni kweli wamehusika na matukio hayo tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria, niwaombe tu wananchi wa maeneo hayo waondoe taharuki iliyokuwa mwanzo, waendelee na biashara zao kama kawaida na leo usiku (jana ) nitakwenda na kikosi kazi katika eneo hilo,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imesema inaendelea kumshikilia Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Benson Kigaila kwa kuwa kuna mambo hayajakamilika.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa alisema Kigaila anashikiliwa na jeshi hilo akituhumiwa kutoa lugha zinazolenga kukashifu viongozi wa serikali, serikali pamoja na watu wanaofanya kazi na serikali. Alisema jeshi hilo linaendelea kumshikilia na anaendelea na mahojiano na upelelezi utakapokamilika, atafikishwa mahakamani.
Polisi waliopiga raia Ukonga kuchukuliwa hatua Polisi waliopiga raia Ukonga kuchukuliwa hatua Reviewed by Zero Degree on 10/25/2017 11:21:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.