Loading...

Ajali yaua wanne mkoani Morogoro

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei
Watu wanne wamefariki dunia baada ya magari mawili ya mizigo kugongana uso kwa uso katika eneo la Sangasanga wilayani Mvomero.

Miongoni mwa waliokufa katika ajali hiyo iliyotokea katika barabara kuu ya Morogoro – Iringa ni madereva wa magari hayo.

Ajali hiyo imetokea leo Jumamosi Novemba 4,2017 saa nne asubuhi ikihusisha lori aina ya Fuso lililokuwa limebeba viazi na Scania lililokuwa limebeba shehena ya mafuta ya chakula.

Mbali ya madereva wa magari hayo, wengine waliokufa ni utingo wa Fuso na mwanamke aliyekuwa abiria kwenye lori hilo.

Imeelezwa Scania lilikuwa likiendeshwa na Almas Halfan mkazi wa Dar es Salaam.

Walioshuhudia ajali hiyo wamesema Fuso lilikuwa likijaribu kuyapita magari mengine ndipo lilipogongana uso kwa uso na Scania.

Mohamed Chuo aliyeshuhudia ajali hiyo amesema dereva wa Fuso hakuwa makini katika kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake na alikuwa katika mwendo mkali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei akizungumzia ajali hiyo amesema imesababishwa na uzembe wa dereva wa Fuso.

Amesema majina ya wengine waliokufa bado hayajapatikana. Kamanda Matei amewaonya madereva kuwa makini wanapokuwa barabarani ili kuepuka ajali.



Ajali yaua wanne mkoani Morogoro Ajali yaua wanne mkoani Morogoro Reviewed by Zero Degree on 11/04/2017 06:44:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.