Loading...

Asilimia 90% ya uchafu wa Bahari unatokana na mifuko ya plastiki

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba
UCHAFUZI wa mazingira kutokana na mifuko ya plastiki Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi, bado ni tatizo kubwa huku ikielezwa asilimia 90 ya uchafu Bahari ya Hindi unatokana na mifuko hiyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema maamuzi ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo nchini hayawezi kufanywa na wizara yake pekee.

January alisema uamuzi juu ya jambo hilo unahusu idara na taasisi za Serikali na sekta binafsi. Kutokana na hali hiyo, alisema uamuzi wa pamoja kutoka katika idara na taasisi za Serikali na sekta binafsi ndiyo itakuwa dawa ya kukomesha utengenezaji, uagizaji na matumizi ya mifuko hiyo nchini.

“Asilimia 60 ya mifuko hiyo inatoka nje ya nchi na ina madhara kwa kuwa asilimia 90 ya uchafu baharini unatokana na mifuko hiyo. Kuipiga marufuku lazima uamuzi uwe wa pamoja kutokana na upana wa mawanda yake ambayo yanawahusu watu wa kodi, viwanda, ajira na biashara ya nje,” alieleza January.

Alitoa maelezo hayo baada ya gazeti hili kutaka kupata kauli ya Serikali kutokana na Jiji la Dar es Salaam kuchafuliwa kwa mifuko ya plastiki kufuatia mafuriko yaliyotokea wiki iliyopita. Katika maeneo kadhaa ya jiji hilo, kuna uzagaaji mkubwa wa takataka za mifuko ya plastiki baada ya mafuriko kutokea.

Mbali na uchafuzi wa mazingira, Waziri huyo alisema mifuko hiyo inapokaa kwenye maji kwa muda mrefu husagikasagika na kuwa katika chembechembe ndogo ndogo ambazo samaki huwa wanazila.

Alisema kutokana na hali hiyo, watu hula chembechembe hizo za mifuko pale wapokula samaki hao, lakini pia mifuko hiyo ina madhara kwa mifugo kama vile ng’ombe ambao hufa wanapoila mifuko hiyo. Kwa upande wake, Ofisa Mazingira Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Fikiri Kenyela alisema mifuko ya plastiki ikichomwa inatoa sumu nyingi kama vile ‘dioxin’ ambayo ina madhara kwa binadamu.

Pia mtu anaweza kupata madhara ya saratani endapo itatumika kuwekea chakula cha moto kama vile chipsi na huathiri mfumo wa uzazi hasa kwa akina mama kutokana na kuathiri mfumo wa homoni. Madhara mengine ya mifuko hiyo ni kuathiri ardhi kwa kuwa haiozi na hivyo kuathiri shughuli nyingine za kiuchumi kama vile kilimo, kina cha maji, mazalia ya samaki na kuua viumbe hai kwa kukosa hewa.

January alisema Sheria ya Mazingira inataka ushirikishwaji wa wadau wengine ndiyo maana miezi mitatu iliyopita walikuwa na kikao Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kujadili mambo ya mazingira. Baadhi ya wadau waliohudhuria mkutano huo ni wa sekta ya viwanda, mazingira na watu wa Serikali. Pamoja na changamoto hiyo, alisema jambo hilo linasubiri maamuzi ya mwisho ya Baraza la Mawaziri.
Asilimia 90% ya uchafu wa Bahari unatokana na mifuko ya plastiki Asilimia 90% ya uchafu wa Bahari unatokana na mifuko ya plastiki Reviewed by Zero Degree on 11/01/2017 01:04:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.