Loading...

Mugabe ang'atuka rasmi

Rais Robert Mugabe ajiuzulu
Spika wa bunge la Zimbabwe, Jacob Mudenda ametangaza kuwa rais Robert Mugabe amejiuzulu.

Mudenda alisema kuwa hatua hiyo ni ya kujitolea na amefanya hivyo ili kuweza kuwepo kwa mabadiliko ya amani ya mamlaka kulingana na chombo cha habari cha Reuters.

Tangazo hilo la ghafla lilizuia harakati za bunge kutaka kumng'oa madarakani ambazo zilikuwa zimeanza dhidi yake.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Reuters, Spika wa bunge amesema kuwa kiongozi mpya atawekwa madarakani siku ya Jumatano.

Wabunge walifurahia kufuatia hatua hiyo na raia wameanza kusherehekea barabarani.

Awali bwana Mugabe alikuwa amekataa kujiuzulu licha ya jeshi kuchukua mamlaka huku hatua hiyo ikifuatiwa na maadamano ya raia waliotaka kiongozi huyo kung'atuka mamlakani wiki hii.

Amekuwa madarakani tangu taifa hilo lijipatie uhuru wake 1980.

Bwana Mugabe ameshinda uchaguzi wa urais mara kadhaa lakini katika kipindi cha miaka 15 iliopita shughuli hiyo imekumbwa na ghasia dhidi ya wapinzani wake.

Ameongoza kipindi cha uchumi ulioanguka ambapo raia wamezidi kuwa masikini zaidi ya walivyokuwa 1980.

Kilichosababisha kung'atuliwa madarakani kwa kiongozi huyo ni pale alipoamua kumfuta kazi makamu wake, Emmerson Mnangagwa wiki mbili zilizopita.

Hatua hiyo ilionekana na wengi kama ya kutaka mkewe kumrithi.

Iliwaudhi viongozi wa jeshi ambao waliingilia kati na kumweka rais Mugabe katika kizuizi cha nyumbani.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amesema kuwa kujiuzulu kwa Mugabe kunaipatia Zimbabwe fursa ya kuwa na mwanzo mpya kufuatia ukandamizaji uliotawala uongozi wa Mugabe.

Amesema kuwa Uingereza ambaye ni rafiki wa zamani wa Zimbabwe atafanya kila awezalo kusaidia kufanyika kwa uchaguzi ulio huru na haki na kujenga uchumi wa Zimbabwe.

Ubalozi wa Marekani mjini Harare umesema kuwa ni hatua ya kihistoria na kuwapongeza raia wa Zimbabwe kwa kutoa sauti zao na kusema kwa njia ya amani kwamba ni wakati wa mabadiliko.

Chama cha upinzani nchini Afrika Kusini cha Democratic Alliance kilifurahia hatua hiyo kikisema kuwa bwana Mugabe alibadilika kutoka kuwa mkombozi hadi dikteta.

Kwa mujibu wa taarifa ya BBC, mwanaharakati wa haki za kibinaadamu Linda Masarira alisema: ''Ninafuraha sana leo kwa sababu nimekuwa nikiamini kwamba Mugabe atajiuzulu katika maisha yangu na imefanyika''.

''Na sasa kwenda mbele ni wakati wa upinzani kujiandaa na kuona kwamba tunakuwa na serikali inayowajali raia wake.Na kila mtu lazima ashirikishwe''.
Mugabe ang'atuka rasmi Mugabe ang'atuka rasmi Reviewed by Zero Degree on 11/22/2017 03:06:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.