Loading...

Rais Magufuli, Mseveni watilia mkazo ujenzi wa bomba la mafuta


RAIS John Magufuli ametaka ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga ukamilike mapema kabla ya mwaka 2020 ili uzalishaji wa mafuta uanze.

Rais Magufuli ambaye yupo nchini Uganda kwa ziara ya kikazi ya siku tatu alisema hakuna sababu ya kuchukua muda mrefu kwa sababu mkandarasi anaweza kufanya kazi kwa saa 24, lakini pia kazi hiyo inaweza kugawanywa kwa wakandarasi 10 kila mmoja ajenge kilomita 145.

Kauli hiyo aliitoa jana alipoungana na Rais Yoweri Museveni wa Jamhuri ya Uganda katika uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi huo. Jiwe hilo liliwekwa kwenye kijiji cha Luzinga, mkoa wa Rakia nchini Uganda baada ya uzinduzi kama huo kufanyika kwanza Chongoleani, mkoani Tanga, Agosti 05, mwaka huu.

“Wataalamu wa Tanzania na Uganda mkae pamoja ili kuhakikisha ujenzi wa bomba hili lenye urefu wa kilomita 1,445 unakamilika kabla ya mwaka 2020. Mnaweza hata kuweka wakandarasi 10 ili kazi iishe hata mwaka 2019,” alieleza Rais Magufuli na kushangiliwa.

Bomba hili litajengwa na kuendeshwa na Kampuni ya Bomba la Mafuta kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (NOC), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni tatu za mafuta za CNOOC, TOTAL na TULLOW kwa gharama ya dola za Marekani bilioni 3.5.

Alisema mradi huo ni mwarobaini kwa uchumi wa nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa utatoa ajira kwa watu wengi wakati na baada ya ujenzi. Aliwataka wananchi wa Uganda na Tanzania kutoa huduma muhimu kama zinazotakiwa katika mradi huu kwani utawainua kimaisha.

“Huu ni wakati kwa wananchi wa nchi hizi mbili kupata fedha kutokana na uwepo wa mradi huu mkubwa utakaoajiri wengi,” alisema.

Mradi huo ambao gharama zake za ujenzi ni takribani Sh trilioni nane za Tanzania utapita mikoa minane ya Tanzania; wilaya 24, vijiji 134 na vitongoji 210, lakini pia kuajiri zaidi ya watu 10,000. Uganda bomba hilo litapita wilaya nane.

Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dk Medard Kalemani alisema ujenzi wa bomba hilo utaenda sambamba na ujenzi vituo sita vya kusukuma mafuta, vituo viwili vya kupunguza spidi na mgando wa mafuta, valvu 53, matangi makubwa matano yanayoweza kubeba mapipa laki tano kila moja na kuhifadhi mapipa milioni 2.5.

Waziri wa Nishati wa Uganda, Irene Muloni alisema mradi wa bomba hilo utaleta maendeleo sekta ya miundombinu kama barabara na kuinua biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Bomba hilo litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 kwa siku ambapo kilomita 1,115 zitakuwa upande wa Tanzania na kilomita 330 zitakuwa upande wa Uganda. Rais Magufuli aliyeongozana na mkewe, Mama Janeth, jana waliwasili Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda alikopokewa na Museveni na kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride lililoandaliwa kwa heshima yake.


Wakiwa mpakani hapo yeye na mwenyeji wake walifungua kituo cha pamoja cha huduma za mpakani (One Stop Border Post - OSBP) kilichojengwa kurahisisha taratibu za kiforodha, uhamiaji na kuharakisha biashara mpakani hapo. Habari zaidi zinasema, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Abdallah Mussa kwa kushindwa kumudu majukumu.
Rais Magufuli, Mseveni watilia mkazo ujenzi wa bomba la mafuta Rais Magufuli, Mseveni watilia mkazo ujenzi wa bomba la mafuta Reviewed by Zero Degree on 11/10/2017 09:23:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.